MMOJA wa majeruhi watano waliokuwa wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama kutokana na kufukiwa na kifusi cha mchanga na kukaa siku 41 chini ya mgodi na kuokolewa, Onyiwa Kaiwao (55) amefariki dunia.
Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Joseph
Ngowi amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kusema kuwa chanzo cha
mauti hayo ni kutokana na majeruhi huyo kutapika akiwa amelala hali
ambayo ilifanya matapishi hayo kuingia katika njia ya hewa.
Dk
Ngowi alisema Kaiwao alifariki jana saa sita mchana na kuongeza kuwa
pia alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa nimonia unaosababishwa na baridi kali hali iliyomfanya kutokuwa katika hali ya kawaida tofauti na wenzake.
Hata
hivyo, Dk Ngowi alisema majeruhi huyo pia alikuwa na matatizo katika
utumbo, na hivyo kila akienda haja kubwa alikuwa akitoa magome ya miti
waliyokuwa wakiyatumia kama chakula wakati wakiwa chini ya ardhi.
“Jana
(juzi) tuliwachukua vipimo waathirika wote watano na kuonesha kuwa hali
zao ni nzuri, lakini Onyiwa alionesha kutokuwa na maendeleo mazuri
tofauti na wenzake na ghafla akiwa amelala alijitapikia hali ambayo
matapishi hayo yaliingia katika mirija ya hewa na kuziba hali
iliyosababisha kifo chake,” alisema Dk Ngowi.
Alisema
hali za majeruhi wengine wanne zinaendelea vizuri, na wanaendelea na
mazoezi huku wakila wenyewe hali ambayo wamepanga kesho kuangalia
uwezekano wa kuwafanyia vipimo kwa mara nyingine tena.
Aidha,
Dk Ngowi alisema endapo hali zao hazitakuwa nzuri na kubadilika,
watawahamishia katika Hospitali ya Rufaa kwa ajili ya uangalizi wa juu
hali ambayo watapata mabadiliko zaidi ya afya zao.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Shigitwa (SHIGOMIKO), Hamza Tandiko
alisema wakiwa wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Nyangalata wamekipokea kwa
masikitiko makubwa kifo cha mwenzao na kuwataka waliobaki kutokata tamaa
Mungu atawasaidia watapata nafuu.
“Sisi
kama wachimbaji hatupingani na Mwenyezi Mungu tulijitahidi kadri ya
uwezo wetu kuokoa maisha yao kwa kushirikiana na uongozi wa Hospitali ya
Wilaya, lakini kwa mapenzi ya Mungu ameamua kumchukua Onyiwa akapumzike
na hakuna mtu anaweza kuzuia kifo,” alisema Tandiko.
Wachimbaji
hao wadogo watano waliokolewa kutoka katika mgodi huo wiki iliyopita
baada ya kukaa kwa siku 41 kutokana na kufukiwa na kifusi. Mwenzao mmoja
alifia mgodini wakati wakisubiri majaliwa ya kuokolewa.
Mpekuzi blog
0 Comments