![](https://lh3.googleusercontent.com/blogger_img_proxy/AEn0k_vV1iKi2eFe4rHim1l38snoEjqG58VR2QJCNVCy7QFJdZObFsG8ra3aaKR7jK3lyfn_VE0gzI3FJxrCcNsApgqLnn-NtI25DNAo8kcSEPci9KnCymAjhGz8biqnpKgKMZ_YU24GiU278B_3HM--bZH0cH23rKrAmH45b7k2nuGlrUtExsLtKe3k0Q=s0-d) |
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akijibu maswali ya papo kwa hapo bungeni,
Dodoma hivi karibuni na kuweka wazi mshahara wake. Picha na Maktaba. |
Mzimu wa kung’olewa unazidi kumwandama
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda huku Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali
(NCCR), akitaka Bunge lipige kura ya kutokuwa na imani naye.
Akizungumza bungeni mjini Dodoma jana, mbunge huyo
alienda mbali zaidi na kuomba Naibu Spika, Job Ndugai kuwaongoza
wabunge kupiga kura hiyo ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.
Pia alitaka kung’olewa kwa Waziri wa Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia akisema haiwezekani
aendelee kuwepo wakati fedha za wafadhili zinaliwa bila yeye kuchukua
hatua.
Mkosamali anakuwa mbunge wa tatu kupendekeza
kung’olewa kwa waziri mkuu, akitanguliwa na Mbunge wa Mwibara, alphaxard
Lugola (CCM) na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR).
Mkosamali alisema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinaonyesha hakuna ufuatiliaji wa fedha
zinazoidhinishwa na Bunge na kupelekwa katika Halmashauri nchini.
Alisema taarifa zinaonyesha asilimia 20 ya bajeti
ya Serikali huingia mifukoni mwa watu na kuongeza kuwa hata Bunge
likapitisha bajeti ya Trilioni 40 bado asilimia 20 zitakwenda mifukoni
mwa watu.
Mkosamali alisema katika semina mbalimbali wabunge
walielezwa kuwa taarifa za CAG zinazofichua ufisadi wa kutisha pamoja
na taarifa za Kamati za Bunge zimekuwa hazifanyiwi kazi na Serikali.
Mbunge huyo aliwasihi wabunge wenzake kuchukua
hatua na kuhakikisha kuwa kabla ya kumalizika kwa mkutano wa 14 wa Bunge
unaoendelea mjini Dodoma mawaziri kadhaa wawe wameng’oka.
Akinukuu Ibara ya 52 ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Mkosamali alisema, Waziri Mkuu ndiye
atakuwa na madaraka ya juu katika udhibiti na usimamizi wa Serikali.
Aliongeza kusema “Kwa nini tusipige kura ya
kumwondoa?... Mheshimiwa Naibu Spika wewe kama kiongozi wetu ndio
unapaswa kutuongoza kupiga kura ya kuwaondoa hawa watu.”
Mkosamali alisema wabunge wanatoa mapendekezo hayo
kwa vile wameshindwa kufanya kazi ambayo walipatiwa na kusisitiza kuwa
wameshawapima na kubaini kuwa hawawezi kazi tena.
“Hatuna chuki na mtu….Hata tukiwaambia tunajua
hamtafanya tumeshawapima tunajua hamtaweza sasa tunawashauri nini tena?”
alihoji Mkosamali wakati akijenga msingi wa hoja yake hiyo.
mwananchi
0 Comments