Mkuu wa wilaya ya Kahama Benson Mpesya akiongoza shughuli ya upandaji wa mahindi katika shamba la halmashauri ya Ushetu wilayani humo |
WANANCHI Wilayani Kahama
Mkoani Shinyanga, wametakiwa kuhifadhi mazao ya chakula na kulima kilimo chenye
tija kwa kuzingatia ushauri wa serikali na maelekezo kutoka kwa wataalamu wa
kilimo ili kunufaika na kilimo chao.
Wito huo umetolewa leo na
Mkuu wa wilaya ya Kahama, Benson Mpesya kwenye upandaji wa mahindi katika
shamba la mfano kwenye maaadhimisho ya miaka 52 ya uhuru, ambayo Kiwilaya
yamefanyika Kitongoji cha Kalaba, kata ya Kisuke.
Mkuu wa wilaya ya kahama Benson Mpesya Akizungumza na Waandishi wa Habari |
Amesema wakulima wengi
wamekuwa hawafahamu umuhimu wa kupanda mazao kwa nafasi ili kupata mavuno bora,
hivyo halmashauri ya Ushetu imeamua kutoa elimu ya upandaji wa mazao ili
wakulima walime kilimo chenye tija.
Mpesya ambaye alikuwa Mgeni
rasmi katika maadhimisho hayo, amesema kwa kufanya hivyo mkulima ataweza kupata
magunia 25-30 ya mahindi katika hekta moja, na kumtoa katika hali ya umasikini
ya kutegemea misaada ya chakula kila mwaka.
Mkuu wa Wilaya akiwa na baadhi ya Wanafunzi wa shule ya msingi Kisuke walioshiriki upandaji huo wa Mahindi |
Katika hatua nyingine Mpesya
amegawa miti kwa ajili ya kutunza mazingira kwa wananchi, Walimu pamoja na
wanafunzi wa shule ya msingi Kisuke, baada ya kushiriki katika zoezi la
upandaji wa Mahindi katika hekari moja ya mfano.
Mkuu wa wilaya akikabidhi miche ya miti kwa wananchi na watu wote walioshiriki shughuli hiyo |
Awali akimkaribisha Mgeni
Rasmi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu, Isabella Chilumba amesema lengo la
kuotesha mahindi katika maadhimisho hayo ni kuhamasisha kilimo cha kisasa na
chenye tija ili kukabiliana na tatizo la Njaa wilayani Kahama.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu, Isabella Chilumba akiongea na Waandishi wa Habari |
Chilumba amesema wanatarajia
kuendelea na uapandaji huo ili kukamilisha hekari 40 za Mahindi, Alizeti na
mazao mengine, na chakula hicho kugawanywa katika shule mbalimbali wilayani
kahama katika mpango wa kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula mashuleni.
Maadhimisho hayo kitaifa
yamefanyika katika uwanja wa Uhuru jijini Dar-es-salaam, mgeni rasimi akiwa ni
rais Jakaya Kikwete, na kauli mbiu isemayo “Vijana
ni Nguzo ya Rasilimali Watu, Tuwaamini, Tuwawezeshe na Tuwatumie kwa Manufaa ya
Taifa Letu”.
0 Comments