Mjengo wa staa wa filamu za Bongo,
Elizabeth Michael ‘Lulu’ uliopo Mbezi Temboni-Salanga jijini Dar es
Salaam umeingia kwenye lawama kufuatia madai kwamba, unatumika kwa
kutapeli watu wanaotaka kununua nyumba maeneo hayo.
Mjengo wa staa wa filamu za Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ uliopo Mbezi Temboni-Salanga jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa chanzo chetu ambacho kina
makazi jirani na nyumba hiyo, baadhi ya watu wanaojiita madalali
wamekuwa wakiwapeleka wateja kwa siri kwenye nyumba hiyo ambayo
haijaisha na kusema inauzwa na Lulu mwenyewe.
MCHEZO ULIVYO
“Baadhi ya madalali feki wamekuwa wakiwaleta wateja wanaotaka kununua nyumba maeneo haya. Wakifika wanasema Lulu anaiuza, wakiwa wameshaiona wanatoa fedha za usumbufu au za kuwapoza wasipeleke watej wengine na kutoa namba feki ya Lulu ili mteja ampigie.
“Wapo wateja walishanifuata na kusema wanampigia Lulu hapatikani, lakini waliponionesha namba yenyewe si ya Lulu.
“Siku moja mteja mmoja aliletwa na
dalali kuiona nyumba, akaipenda, akampa dalali shilingi 300,000 za
kumfanya asipeleke wateja wengine, akampigia Lulu hakupatikana.
Alipokuja kwangu nikaiangalia namba hiyo ilisajiliwa kwa jina la
Mwanahamis nani sijui,” kilisema chanzo hicho.
MAPAPARAZI WAJIFANYA WATEJA, MADALALI WASHTUKA
Mwishoni mwa wiki iliyopita, mapaparazi wetu walijifanya wateja wa kuinunua nyumba hiyo na kwenda kukutana na watu wawili waliodaiwa kuwa ndiyo madalali, Kitwana na Mambeze ‘Mchopa’.
Baada ya mazungumzo, madalali hao
walidai kuwa, funguo za kuingia ndani ya nyumba hiyo anazo mama Lulu
(Lucresia Karugila) na alisema angefika siku hiyo saa kumi jioni na
kuwataka mapaparazi kurudi muda huo.
Wakati mapaparazi wetu wanaondoka,
dalali mmoja alisema: “Nyie kama mmekuja kututega mmeliwa wenyewe, hapa
hakuna mtoto wa kijijini. Wanaokuja hapa kutaka nyumba wanajulikana,
nyie mmetumwa.”
LULU ALISHAFIKA, HAJUI KITU
Sosi mwingine alisema hivi karibuni alimuona Lulu akifika eneo hilo kwa ajili ya kuangalia nyumba hiyo ambayo imesimama ujenzi lakini hakuweka wazi kama alikuwa na nia ya kuiuza!
“Mimi mara ya mwisho nilimuona Lulu eneo
hili na gari lake, naona alikuja kuangalia nyumba inaendeleaje na
usalama pia. Mambo ya kuwa anaiuza hata siyajui ingawa kweli hata mimi
nimekuwa nikiwaona watu wakija,” alisema sosi huyo ambaye hakutaka jina
lake lichorwe gazetini.
Juzi, gazeti hili lilimsaka Lulu kwa njia ya simu kwa ajili ya kumuuliza kuhusu suala hilo ambapo, awali aling’aka, akasema:
“Wewe ndiyo unaniambia kusema ukweli,
sijui chochote. Naomba mnipe habari kwa upana ilivyo maana nyie
waandishi mara nyingi mnakuaga wa kwanza kujua habari kuliko mhusika.”
Amani: Wewe Lulu sema ukweli tu, kama unaiuza. Nilichokwambia ndicho.”
Lulu: Kweli mimi siiuzi nyumba yangu wala sina wazo. Huyo aliyewapa habari awape kwa undani ili nijue.”
0 Comments