Aliyejeruhiwa ni mhudumu wa nyumba ya wageni ya kanisa hilo, Benadeta Alfred (25) aliyekumbwa na mkasa huo juzi saa mbili usiku.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino
Mlowola alisema jana kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa ni bomu
la kutengenezwa kienyeji linalojulikana kwa jina la IED na kwamba
uchunguzi unaendelea kuwabaini walioliweka kanisani.
Mlowola alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa
polisi wanapoona vitu ambavyo wanavitilia shaka ili uchunguzi wa
kitaalamu ufanyike kabla ya kusababisha madhara.
Mlinzi wa kanisa hilo, Charles Mathayo alisema
walisikia kishindo kikubwa cha mlipuko na baada ya muda mfupi wakasikia
kelele za mhudumu huyo akiomba msaada.
Alisema walipofika eneo la tukio, walimkuta akiwa
ameanguka huku akitokwa damu sehemu mbalimbali za mwili pembeni mwake
kukiwa na vitu ambavyo alisema hakuvifahamu. Shuhuda mwingine,
mwanafunzi wa Chuo cha Kompyuta kanisani hapo, Erina Emmanuel alisema
walisikia mlipuko, baadaye wakasikia sauti ya mtu akiomba msaada, lakini
kutokana na hofu walikimbia hawakwenda kumsaidia.
Lilifungwa kama zawadi
Kiongozi mmoja kanisani hapo ambaye hakutaka
kutajwa jina, alisema kitu hicho kilicholipuka kilikuwapo kanisani hapo
tangu Ijumaa iliyopita, kikiwa kimewekwa juu ya makreti ya soda.
Alisema wahudumu walipuuza wakidhani ni mzigo wa
mtu aliyekuwa ameusahau kutokana na jinsi ulivyokuwa umefungwa vizuri
kwa karatasi za zawadi.
Alisema baada ya kuona bahasha hiyo imekaa muda
mrefu bila kuchukuliwa, mhudumu huyo aliichukua kwa lengo la kuipeleka
kwa uongozi wa kanisa.
Alipoushika, mzigo huo ulilipuka na kumjeruhi usoni na miguuni na kupelekwa Hospitali ya Bugando ambako amelazwa.
Hata hivyo, uongozi wa Hospitali ya Bugando uliwazuia waandishi wa habari kumwona majeruhi huyo.
0 Comments