Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda jana aliwasilisha bungeni, bajeti ya ofisi yake na mfuko wa Bunge
inayofikia Sh5.21 trilioni. Kati ya hizo, Sh5 bilioni zimetengwa kwa
ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika baadaye
mwaka huu.
Hayo yalielezwa bungeni jana na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia wakati wa maelezo kuhusu
kazi zilizotekelezwa mwaka 2013/2014 na mwelekeo wa kazi
zitakazotekelezwa 2014/2015.
Ghasia alisema shughuli zitakazogharimiwa na fedha
hizo ni pamoja na maandalizi ya masanduku ya kupigia kura, kupitia
kanuni za uchaguzi na kuandaa fomu na nyaraka mbalimbali za uchaguzi.
Shughuli nyingine ni uhakiki wa majimbo ya uchaguzi huo ambayo ni vijiji, mitaa na vitongoji.
Malipo ya wabunge
Katika bajeti hiyo ya Ofisi ya Waziri Mkuu,
Sh132.6 bilioni zimetengwa kwa ajili ya Mfuko wa Bunge la Muungano, kati
yake posho na mishahara kwa ajili ya Bunge (wabunge na watumishi wa
Bunge) ikiwa ni Sh123.94 bilioni.
Kwa mujibu wa nyaraka za bajeti hiyo, wabunge peke
yao wametengewa Sh102.317 bilioni kwa ajili ya mishahara, posho za
vikao na kujikimu na posho za safari ndani na nje ya nchi.
Kwa mwaka wa fedha unaomalizika Juni 30 mwaka huu,
mishahara na posho za wabunge zilitengwa Sh93.37 bilioni, kati ya hizo
posho zilikuwa Sh48.74 bilioni ikilinganishwa na Sh49.526 bilioni
zilizotengwa katika bajeti 2014/2015, sawa na ongezeko la Sh800 milioni.
Usimamizi wa rasilimali watu na utawala ambayo
ndiyo inayohusika na mishahara na posho kwa watumishi wa Bunge kwa mwaka
wa fedha wa 2014/2015, umetengewa Sh21.6 bilioni.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa mishahara ya wabunge imetengewa Sh12.769 bilioni.
Safari za ndani
Posho za safari ndani ya nchi zimetengewa Sh11.192 bilioni wakati zile za safari za nje kwa wabunge zimetengewa Sh9.08 bilioni.
0 Comments