Advertisement

Responsive Advertisement

Bunge laanza leo kwa posho mpya

Bunge la Bajeti linaanza leo mjini Dodoma huku wabunge wakitarajiwa kuanza kulipwa viwango vipya vya posho, ambazo ni Sh300,000 kwa siku sawa na kiwango wanacholipwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.

Kabla ya kufikia uamuzi wa kupandisha viwango hivyo kwa Sh100,000 zaidi, wabunge walikuwa wakilipwa Sh200,000 kwa siku (yaani Sh70,000 kama posho ya kikao (sitting allowance), Sh80,000 posho ya kujikimu (perdiem) na Sh50,000 ya gharama za usafiri).
Nyongeza hiyo kwa kila mbunge kwa siku, sawa na asilimia 50, italigharimu Bunge la Jamhuri ya Muungano kiasi cha Sh18.5 bilioni kwa siku 52 zilizotengwa kwa ajili ya Bunge la bajeti linalotarajiwa kuhitimishwa Juni 27.
Januari mwaka 2012, Rais Jakaya Kikwete alikataa maombi ya Bunge ya kutaka nyongeza ya posho ipande hadi Sh330,000 na badala yake wabunge hao wakapata nyongeza ya Sh50,000 tu kwa ajili ya usafiri.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililla alipoulizwa kuhusu nyongeza hiyo, hakuthibitisha wala kukanusha, lakini akafafanua kwamba hilo ni suala la uongozi wa Bunge na si la kiutendaji.
“Suala la malipo kuongezeka au kutoongezeka kimsingi siyo kazi ya Ofisi ya Katibu wa Bunge, vipo vyombo vya juu vya uongozi wa Bunge; Kamati ya Uongozi na Tume ya Huduma za Bunge, na vyombo vyote vinaongozwa na Spika. Kwa hiyo, kama kuna nyongeza, sisi tunapewa taarifa tu kwa ajili ya kutekeleza,” alisema Dk Kashililla na kuongeza:
“Hadi sasa sina taarifa rasmi kuhusu suala hilo, ikiwa litafika mezani kwangu kama maelekezo, tutatekeleza kwa mujibu wa maelekezo husika.”
Habari ambazo zimelifikia gazeti hili kutoka vyanzo mbalimbali ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinasema, uongozi wa muhimili huo umeamua kuanza kulipa kiasi hicho cha fedha kutokana na shinikizo kubwa kutoka kwa wabunge.
Taarifa za kuwapo kwa msukumo wa ajenda ya kupandisha posho za wabunge zilianza kusikika wakati Bunge la Katiba likielekea ukingoni, wakati wabunge walikuwa wakihoji sababu za wajumbe kulipwa kiasi kikubwa cha fedha kwa kazi ileile na katika mazingira yaleyale, wakati wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wakilipwa kiasi kidogo.
“Msingi wa hoja yetu hapa ni kwamba maisha na mazingira ya Dodoma ni yale sasa, leo kwanini wajumbe wa Bunge la Katiba walipwe Sh300,000 sisi tulipwe kidogo kuliko hicho?” alihoji mmoja wa wabunge.
“Na usisahau mwanzoni tu pale (mbunge wa Sumve, Richard) Ndassa alitoa hoja akisema posho hiyo ya Sh300,000 haitoshi kwa kuwa gharama za maisha Dodoma zimepanda... Gharama haziwezi kupanda Bunge la Katiba pekee.”
Mbunge huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema kama kigezo ni gharama za maisha, mazingira hayo ndiyo wanayokutana nayo wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.

 

Post a Comment

0 Comments