Makamu wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad jana alikuwa miongoni
mwa maelfu ya waumini wa Kiislamu waliojitokeza kumzika Sheikh Hassan
Ilunga aliyefariki dunia Dar es Salaam juzi kwa maradhi ya kupooza.
Hamad ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF aliongozana
na Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba katika ibada ya kuaga mwili
wa sheikh huyo, kabla ya maziko yaliyofanyika kwenye Makaburi ya
Mwinyimkuu, Magomeni Mapipa.
Akizungumza kabla ya ibada ya maziko, Amiri wa
Shura ya Maimamu, Sheikh Mussa Kundecha alisema marehemu alipata
matibabu ya figo huko India na Aprili mwaka huu alirejea nyumbani.
“Akiwa huko (India), alianza kutokewa na matatizo
mapya ikiwa ni pamoja na baadhi ya viungo vyake kupooza au sijui tuseme
kufa ganzi na mara ikawa leo mguu kesho unarudi hali ya kawaida na hali
hiyo ikawa inajirudiarudia,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, Sheikh Kundecha alisema
madaktari hawakubaini ugonjwa uliokuwa unamsumbua ndipo alipopewa ruhusa
ya kurudi nchini.
“Aliporudi alikuwa anazungumza vizuri na
kuwasiliana bila shida na watu wengine, ingawa kuanzia katika kiuno
kwenda chini viungo havikuwa na mawasiliano mazuri na mwili,” alisema na
kuongeza kuwa siku tatu kabla ya mauti alipoteza fahamu.
0 Comments