CHAMA cha Alliance for Change and
Transparency (ACT-Tanzania), jana kilikabidhiwa cheti cha usajili wa
kudumu na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.
Jaji Mutungi alikabidhi cheti hicho
mjini Dodoma jana kwa Kaimu Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Kadawi
Limbu na kuwataka viongozi wa chama hicho kufanya siasa zenye ukomavu
kwa kuzingatia Sheria ya Vyama vya Siasa.
Aliwataka viongozi wa chama hicho,
kuheshimu wanachama wao kwani vyama vingi vikishapata usajili, viongozi
wake wanaanza kujiona wanajua kuliko wanachama wao.
“Mmepata usajili huku nchi ina amani,
fanyeni siasa zitakazohakikisha nchi inaendelea kuwa na amani,” alisema
Jaji Mutungi na kutaka chama hicho kushiriki kutoa maoni kuhusu
marekebisho Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi.
Msaidizi wa Msajili wa Vyama vya Siasa,
Sisty Nyahoza, alipongeza ACT kwa kutimiza masharti yote ya kupata
usajili wa kudumu na kuongeza kuwa chama hicho kilifanikiwa kupata
wanachama zaidi ya 200 katika mikoa 10 ya Tanzania Bara na mikoa miwili
kutokea Zanzibar.
Aliwataka viongozi wake kufahamu kwamba
sasa wako chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Gharama za
Uchaguzi na kuwataka kuepuka ushindani na vyama vingine unaoweza
kusababisha wasahau sheria zinazoongoza vyama vyao.
“Epukeni kujihusisha katika vurugu,
Sheria inakataza vyama vya siasa kutumia nguvu katika siasa, hali hiyo
inafifisha demokrasia na kuwatia hofu wanachama,” alisema Nyahoza.
Aliwataka kuepuka migogoro ya ndani ya
chama chao kwakuwa mara nyingi vyama vya siasa vinapotafuta, viongozi
wake wanakuwa pamoja, wakishapata wengine wanaota mapembe. Limbu alisema
chama hicho kimepanga kuonesha demokrasia ya kweli nchini na hakitakuwa
chama cha vurugu.
“Chama hiki kitakuwa chama cha heshima,
hakitakuwa na mmiliki kitakuwa cha wanachama, hatutegemei migogoro na
tutafanya siasa za kistaarabu,” alisema.
Alisema chama hicho kitashiriki
kikamilifu kufanyia maboresho Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria
Gharama za Uchaguzi, ikiwemo kuhakikisha Ofisi ya Msajili wa vyama vya
siasa inakuwa na meno kwa vyama vya siasa,” alisema Limbu.
Kuhusu chama hicho kuwa na watu maarufu
nyuma yake, Limbu alisema hayo ni masuala ya kusikika sio kweli kwani
wao ni wanasiasa wazoefu, wanajiamini na hakuna sababu ya kufanya kazi
kwa kuwa kuna watu nyuma yao.
“Kuna watu na viongozi wa vyama vingine
wanakerwa na demokrasia ndani ya vyama vyao, vipo vyama ambavyo ni
kampuni ya watu, ukionekana kugusa maslahi ya mtu unafukuzwa
tunawakaribisha waje tujenge demokrasia ya kweli,” alisema Limbu.
0 Comments