WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano
na Uratibu, Stephen Wassira amesema viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF)
hawayatambui Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Pia, amesema baadhi
ya wajumbe wake, wanapinga Siku ya Mapinduzi, kutambuliwa katika kalenda
za kitaifa nchini kote.
Wassira alisema hayo katika mkutano wa hadhara, uliofanyika katika Uwanja wa Kibandamaiti mjini Zanzibar.
Alisema chama hicho hakina dhamira na nia nzuri kwa Wazanzibari katika Mapinduzi ya Januari mwaka 1964.
Akifafanua, alisema alipambana na
viongozi wa CUF wakati wakijadili Katiba katika Bunge Maalumu la Katiba
na kuwaeleza umuhimu wa Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo ndiyo
yaliyowakomboa wananchi wa Zanzibar kutoka katika makucha ya wakoloni.
Kwa mfano, Wassira alimtaja mmoja wa
wajumbe waliokuwemo katika kamati yake, ambayo yeye alikuwa kiongozi
kuwa ni Ismail Jussa, ambaye alikuwa akipinga na kutaka siku ya
Mapinduzi, isitambuliwe na kufanywa kuwa siku ya mapumziko kitaifa.
Alisema Jussa anataka siku za sherehe za
kitaifa, ikiwemo Mapinduzi ya Januari 1964 na Uhuru wa Tanganyika,
ziondolewe na zisitambuliwe kama siku za kitaifa rasmi.
“Hawa watu ni wa ajabu sana kumbe
hawayatambui Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, kwani hata katika
kamati za Bunge Maalumu la Katiba nilipambana nao kikamilifu huku
wakitaka Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12 mwaka 1964
isitambuliwe rasmi,” alisema.
Wassira alisema serikali zote mbili,
tayari zimeanza kuzipatia ufumbuzi kero mbalimbali za Muungano, ambazo
zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi wa Zanzibar.
Hata hivyo, alisema kitendo cha wajumbe
wa Bunge Maalumu la Katiba, wakiongozwa na wapinzani kutoka nje ya
vikao, kwa kiasi kikubwa kutaathiri na kuzipatia ufumbuzi kero za
Muungano.
“Nasikitishwa sana na kitendo cha
wapinzani kutoka nje ya vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, kwa sababu
kutapelekea kero za Muungano zinazoihusu Zanzibar kushindwa kupatiwa
ufumbuzi wake,” alisema.
0 Comments