Rehema Chalamila
(Ray C) akiwa kitandani
Ugonjwa wa homa ya dengue umezidi
kusambaa mkoani Dar es Salaam na sasa umeathiri wilaya zake tatu na
kuzua hofu kwa wananchi.Miongoni
mwa walioathiriwa na homa hiyo ni mwanamuziki maarufu Rehema Chalamila
(Ray C) ambaye amelazwa katika Wodi Namba Tano ya Hospitali ya
Mwananyamala.
Mmoja wa madaktari wa hospitali hiyo, alithibitisha kulazwa
kwa Ray C kutokana na ugonjwa huo jana.“Tumethibitisha
kwamba Ray C ana dalili zote za dengue, lakini kimaadili siruhusiwi
kutoa taarifa za mgonjwa,” alisema daktari huyo ambaye hakutaka kutajwa
jina lake.
Hata
hivyo, waandishi wa gazeti hili walimwona mwanamuziki huyo hospitalini
hapo akiwa katika usingizi mzito na madaktari walisema hakuwa katika
hali mbaya bali alikuwa amelala kwa sababu ya uchovu wa dawa.
Mbali na Ray C, pia madaktari watatu na muuguzi mmoja wameripotiwa kuugua ugonjwa huo.
Tayari
mamlaka zimetoa tahadhari kwa wananchi kuwataka wachukue hatua za
haraka kuzuia maambukizi ya homa hiyo inayosababishwa na mbu
anayejulikana kitaalamu kama aedes egyptiae.
Hadi
sasa wagonjwa zaidi ya 100 wameripotiwa kuugua ugonjwa huo katika
wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke na baadhi wakiripotiwa kupoteza
maisha.
Takwimu
kutoka Kitengo cha Utafiti wa Magonjwa cha Ifakara (IHI), kilichoweka
kambi katika Hospitali ya Mwananyamala kutafiti aina za homa,
zinaonyesha kuwa kwa miezi miwili ya Machi na Aprili pekee, wagonjwa 85
walibainika kuwa na homa hiyo.
Hata
hivyo, idadi inaweza kuwa kubwa zaidi kutokana na kukosekana kwa
takwimu, vipimo na watu kuufananisha ugonjwa huo na malaria.
Daktari
kiongozi wa hospitali hiyo ambaye pia ni mtaalamu wa ugonjwa huo, Dk
Mrisho Rupinda alisema kuwa kuna taarifa za wagonjwa wa dengue
walioripotiwa katika maeneo yote ya Dar es Salaam.
“Katika
kipindi cha wiki moja iliyopita tayari madaktari wawili kwenye
hospitali hii wamebainika kuugua ugonjwa huo, tunahisi walipata
maambukizi kwenye maeneo ya humuhumu ndani hospitali,” alisema Dk
Rupinda.
Alisema
hali ni mbaya kuliko inavyodhaniwa kwa kuwa asilimia zaidi ya 50 ya
wanaopimwa na kubainika kuwa na ugonjwa huo ni watu wazima kuanzia miaka
18.
Hata hivyo, takwimu za walio chini ya umri huo ni vigumu kupatikana kutokana na sampuli zinazopimwa na watafiti IHI.
Dk
Rupinda alisema kuna wataalamu wa kutosha kubaini ugonjwa huo lakini
tatizo kubwa ni vifaa na vitendanishi... “Mgonjwa anapobainika
kuambukizwa dengue hana tiba rasmi, tunakutibu dalili.”
Amana na Temeke
Katika Hospitali ya Temeke jana wagonjwa walikuwa wakihamishwa katika wodi kwa ajili ya kupuliza dawa kudhibiti mbu.
Chanzo
kimoja cha habari katika hospitali hiyo kilieleza kuwa, muuguzi na
daktari mmoja wa hospitali hiyo waligundulika kuwa na homa hiyo.
Mganga
Mkuu wa Hospitali ya Amana, Meshack Shimwela alisema wamekuwa wakipokea
wagonjwa wengi wa homa ya dengue ambao walitibiwa na kuruhusiwa kwa
kuwa hawakuwa mahututi.
“Ni
ugonjwa wa mlipuko ambao huwa mkali kwa mara ya kwanza lakini baada ya
watu kujua jinsi ya kujikinga, hupungua, pia muda ukipita mwili hujenga
kinga wenyewe,” alisema Dk Shimwela na kuongeza:
“Kwa mfano, Aprili kuna kesi zaidi ya nne ambazo ziliripotiwa hapa kwetu.”
Alisema dalili za ugonjwa huo mara nyingi hufanana na zile za malaria kama vile homa kali, maumivu ya kichwa na misuli.
Msimamizi
wa takwimu, maafa na dharura katika Manispaa ya Temeke, Dk Laurent
Chipata alisema hali si shwari: “Kimsingi ugonjwa huu umelipuka kwa
kiwango kikubwa sana kwenye Manispaa ya Temeke na hali ilivyo sasa
inahitaji hatua za haraka kuwanusuru wakazi wake.” Alisema wagonjwa wote
wanaofika wakiwa na homa wanapimwa kikamilifu na wale wanaogundulika
kuwa na ugonjwa huo wamekuwa wakipewa tiba.
Pamoja
na mlipuko huo, alisema hakuna karantini iliyowekwa kwenye maeneo yote,
bali wagonjwa wanaobainika hupewa usimamizi kuwekewa vyandarua kuzuia
maambukizi zaidi.
Muhimbili
Katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ilielezwa kuwa kati ya wagonjwa 10
wanaofika wakiwa na homa, wawili hadi wanne wanakuwa wameambukizwa
ugonjwa huo.
Daktari
wa magonjwa ya dharura na ajali katika hospitali hiyo, Juma Mfinanga
alisema ugonjwa huo ulianza kubainika tangu Machi mwaka huu, hatua
iliyosababisha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuongeza nguvu ya
kupambana nao.
Wizara ya Afya
Taarifa
ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inaeleza kuwa kuanzia Ijumaa wiki
iliyopita hadi jana, wagonjwa 23 waliripotiwa katika Wilaya ya Kinondoni
na sita Ilala.
Msemaji
wa wizara hiyo, Nsachris Mwamaja aliwataka wananchi kujifunza jinsi ya
kujikinga na ugonjwa huo na kuangamiza mazalia ya mbu kwa kufukia
madimbwi ya maji yaliyotuama au kunyunyizia dawa.
Kinga
nyingine alisema ni kuondoa vitu vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama
vile vifuu vya nazi, makopo na magurudumu ya magari, kufyeka vichaka,
kufukia mashimo ya majitaka na kusafisha mazingira kwa jumla.
“Virusi
vya homa ya dengue havina tiba maalumu wala chanjo, bali mgonjwa
hutibiwa dalili zinazoambatana na ugonjwa huo kama vile homa,
kupungukiwa maji au damu,” alisema Mwamaja
0 Comments