KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amemvaa Rais Jakaya Kikwete kuwa ni mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa kwanza kuchochea jeshi lake kufanya mapinduzi ya kijeshi ili kuzuia matakwa ya wananchi juu ya katiba mpya kutekelezwa.
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa na mbunge wa Hai, alisema kuwa Rais Kikwete ndiye aliyeongoza mawaziri wake na viongozi wengine waandamizi wa CCM na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katika kujadili rasimu kwa kutukanana, kudharauliana, kushutumiana, kubezana, kuzomeana na kushinikizana.
“Haijawahi kutokea kwa rais na mkuu wa nchi kuwaasa wajumbe wa Bunge la Katiba kujadili hoja badala ya jazba, halafu huyo huyo kugeuka na kukejeli na kubeza tume aliyoiteua yeye mwenyewe na hivyo kujenga mazingira ya wajumbe wa Bunge hilo kutukanana, kudharauliana, kushutumiana, kubezana, kuzomeana na kushinikizana. Hapa ndipo CCM ilikoifikisha nchi yetu,” alisema.
Mbowe alisema kauli na vitisho hivi vimetolewa hadharani sio ndani ya ukumbi wa Bunge tu, bali pia hata katika nyumba za ibada bila kujali athari zake kwa jamii yenye imani tofauti za kidini.
Kwa mujibu wa Mbowe, kauli za uchochezi za viongozi wa CCM kuhusu mchakato wa katiba, zimeendelea kutolewa nje ya Bunge Maalumu.
Mbowe alisema hayo jana bungeni mjini hapa wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2014/15.
“Katika mkutano wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana kule Unguja Mei 4 mwaka huu, mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), Salmin Awadh Salmin ambaye ni mjumbe wa Bunge maalumu, alisema wawakilishi wa CCM wanajiandaa kuwasilisha hoja binafsi kwenye baraza hilo ili kuwapa nafasi wananchi waulizwe iwapo wanataka kuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema.
Madhumuni ya mchakato huo ni kuvunja Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo iliamuriwa iwepo na kura ya maoni ya Wazanzibari wote na imesaidia kuleta amani na utulivu Zanzibar.
Alisema kuwa hata kauli ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd kwamba Ismail Jussa Ladhu, Mwakilishi wa Mji Mkongwe sio raia wa Zanzibar ni ya kibaguzi, kichochezi na yenye kupandikiza chuki dhidi ya jamii ya watu wenye asili ya Kihindi.
“Kambi rasmi ya upinzani inapenda kumuuliza Waziri Mkuu, kama hii sasa ndiyo sera mpya ya CCM na serikali yake kuivunja Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na kuibua hisia za ubaguzi,” alisema.
Mbowe alipigilia msumari msimamo wa wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kwamba wamekataa kuwa sehemu ya Bunge Maalumu la aina hii na hawatarudi bungeni hadi hapo dhima halisi ya Bunge hilo itakapopatiwa ufumbuzi.
“Kambi ya upinzani inahoji, kama Rais Kikwete hakuwa tayari kukubali maoni ya wananchi katika mchakato wa mabadiliko ya katiba, kwanini yeye na serikali yake wameliingizia taifa hasara ya kutumia mabilioni ya fedha za walipa kodi kugharamia mchakato wa katiba mpya ambao ni wazi yeye na chama chake hawako tayari kukubali matokeo yake?” alihoji.
Maswali yake matano
Akizungumzia matumizi ya fedha zilizotumika kwa ajili ya Bunge la Katiba, Mbowe alisema fedha zote zilizotumika hazikuidhinishwa na Bunge.
“Ukweli ni kwamba hadi sasa Bunge lako tukufu halijui bajeti yote ya Bunge Maalumu, halijui fedha kiasi gani zimetumika kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya miundombinu ya Bunge hili, au kwa ajili ya posho, mishahara na stahili mbalimbali za wajumbe na watumishi wa Bunge Maalumu hadi lilipoahirishwa tarehe 25 Aprili, 2014.
“Aidha, Bunge lako tukufu halina ufahamu wowote juu ya gharama za Bunge Maalumu pale litakaporudi tarehe 5 Agosti, 2014, kuendelea kujadili rasimu ya katiba mpya,” alisema.
Mbowe alisema kuwa Bunge halina ufahamu huu kwa sababu licha ya madai ya wabunge, Serikali ya CCM haijawahi kuleta makadirio ya matumizi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za Bunge Maalumu.
Alisema kuwa mwaka jana wakati Bunge linajadili makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala iliagiza kwamba bajeti ya Bunge Maalumu iletwe bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa.
Mbowe alisema kuwa agizo hilo sio tu lilipuuzwa mwaka jana kwa Serikali ya CCM kutokuleta bajeti hiyo, bali hata mwaka huu, agizo hilo limepuuzwa kwani bajeti ya Bunge Maalumu haipo katika makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Kutokana na hali hiyo, Mbowe alisema kambi ya upinzani inataka kupata majibu ya maswali matano ambayo ni: (i) Je, bajeti ya matumizi ya Bunge Maalumu ni kiasi gani na kwa ajili ya matumizi gani? (ii) Je, ni kiasi gani cha fedha hizo kimeshatumika hadi sasa na kwa ajili ya matumizi gani?
Maswali mengine ni; (iii) Je, ni nani aliyejadili na kupitisha bajeti hiyo? (iv) Je, ni sheria gani iliyotungwa na Bunge lipi iliyoidhinisha matumizi haya ya fedha za umma? (v) Je, ni lini na kwa waraka gani Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliidhinisha matumizi haya?
0 Comments