Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini, anadaiwa kutoa zabuni ya uchapaji wa nyaraka za serikali kwa Kampuni ya Yuko’s Enterprises Ltd ya mkoani Pwani bila kufuata taratibu.
Kwa mujibu wa nyaraka ambazo Tanzania Daima limezipata, Sagini alitumia wadhifa wake kuwazuia makatibu tawala wa mikoa kutochapa nyaraka muhimu nje ya udhibiti wa mpiga chapa mkuu wa serikali.
Mfumo wa uchapaji uliozuiliwa ulikuwa ukitumia utaratibu wa kutafuta wazabuni kwa njia ya kutangaza katika gazeti la serikali.
Hata hivyo, katibu huyo alichukua hatua ya kuandika barua kwa makatibu tawala wa mikoa nchini yenye kumbukumbu Na 2/CAB111/175/01/149 ya Mei 27, 2011, kusitisha utaratibu huo.
Sagini alitoa sababu za zuio hilo kuwa ni kudhibiti uvujaji wa siri za serikali ambao unatokana na uchapaji wa nyaraka muhimu nje ya udhibiti wa mpiga chapa wa serikali.
Nyaraka hiyo iliendelea kutoa maelekezo kuwa pamoja na zuio hilo, lakini ipo baadhi ya mikoa imekuwa ikiendelea kuchapa nyaraka hizo za serikali nje ya udhibiti wa mpiga chapa mkuu.
Alitaja baadhi ya nyaraka hizo ambazo zinaendelea kuchapwa nje ya udhibiti wa mpiga chapa mkuu wa serikali kuwa ni fomu ya taarifa ya takwimu za shule za msingi namba tisa (TSM 9).
Sagini alieleza madhara ya fomu hizo kuchapwa nje ya mpiga chapa mkuu kuwa ni kutofautiana kwa ubora kati ya halmashauri, mkoa mmoja na mwingine.
“Hali hii husababisha fomu hizo kukosa ubora wa kudumu na kuhifadhi kumbukumbu za mwanafunzi kwa muda mrefu, kukosekana kwa utambulisho madhubuti kwa ajili ya kudhibiti vitendo vya udanganyifu na kuwepo kwa mwanya kwa watumishi wasio waaminifu kupata nakala za fomu hizo na kuzitumia kuingiza wanafunzi wasio na sifa za kujiunga na kidato cha kwanza,” alisema.
Katika barua hiyo, Sagini alitoa maelekezo kwa makatibu tawala kutumia ofisi ya mpiga chapa mkuu kuchapa fomu hizo kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014 ambapo zingechapwa na kuwekwa ubora unaostahili.
Baada ya kutoa taarifa hiyo kwa makatibu tawala, Sagini alitoa waraka mwingine wenye kumbu. Na. CAB. 134/332/01/67 ambao unaelekeza kwa kampuni itakayokuwa na jukumu la kufanya kazi hiyo pasipo kutoa zabuni katika upatikanaji wake.
Tamisemi ilipokea barua yenye kumbu. Na. GPC/P. 180/6/VOL. VI/156 ya Machi 20, 2014 kutoka kwa mpiga chapa mkuu wa serikali ikieleza jinsi ofisi yake inavyoendelea kupata barua za maombi kutoka mikoa na halmashauri za wilaya nchini kuhusu upigaji picha na uchapishaji wa haraka wa TSM 9, mitihani ya kidato cha pili na darasa la nne 2014.
“Kutokana na umuhimu, nyaraka hizo zinatakiwa kuandaliwa, kuchapishwa na kusambazwa kwa usalama mkubwa na kwa kuwa mitambo ya mpiga chapa mkuu wa serikali imekuwa na tatizo la uharibifu uliotokana na hitilafu ya umeme, hivyo mpiga chapa mkuu wa serikali ameshauri kazi hizo kwa mwaka huu wa fedha 2013/2014 zikamilishwe na Kampuni ya Yuko’s Enterprises Ltd ya mkoani Pwani ili kutekeleza usalama wa uchapishaji wa nyaraka za serikali (4GSPR),” alisema.
Mchakato huo umeibua utata mkubwa kwa wazaburi wakipinga utaratibu uliotumika kutoa zabuni hiyo kwa kuwa unatia shaka kutokana na kutotangazwa kwa wazubuni wengine.
Hatua imeibua madai kuwa kampuni hiyo imekuwa ikipewa kazi za uchapaji wa nyaraka za serikali kama fomu ya taarifa ya takwimu za shule za msingi namba tisa (TSM 9), mitihani ya kidato cha pili na darasa la nne 2014.
Sagini hakupatikana kujibu tuhuma hizo kutokana na simu yake kuita bila kujibiwa na hata alipoandikiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) hakuujibu.
0 Comments