KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amekifananisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mchezo wa ‘Mbugi’.
Wakati Mbowe akiwaita CCM Mbugi, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba aliwaita CCM Intarahamwe.
Kwa mujibu wa Mbowe, Mbugi ni mchezo wa soka usio na sheria, wala refa.
Alisema kwenye mchezo wa Mbugi hakuna idadi kamili ya wachezaji, kila
mchezaji akiingia anachezea timu anayotaka, katikati ya mchezo anaweza
kubadilisha timu na kuchezea timu nyingine.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza Baraza jipya la
Mawaziri Kivuli lenye ya wajumbe wa UKAWA, Mbowe alisema wanachosema na
kufanya CCM kwa sasa ni sawa na Mbugi, kwani hawana kanuni na kila mtu
anaweza kusema anachotaka.
Alisema hivi karibuni kumekuwa na kauli na misimamo tofauti kuhusu UKAWA zinazotolewa na viongozi mbalimbali wa chama hicho.
Akitolea mfano alisema hivi karibuni Kamati Kuu ya CCM ambayo Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda ni mjumbe, wamepitisha azimio la kutoshughulika na
UKAWA kwani wameamua kutoka kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
“Pinda huyo huyo akihitimisha hotuba yake, anawasihii UKAWA kurudi
bungeni. Juzi Waziri wa Ofisi ya Rais (Mahusiano), anasema UKAWA
walitoka bila sababu, watarudi bila sababu, lakini ukimsikiliza Nape
Nnauye na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana wanasema UKAWA
wasibembelezwe, waachwe wabaki nje ya Bunge. Hii ni Mbugi.
“Kinana kaja kavua shati kaingia kwenye Mbugi, Nape naye Mbugi,
Wassira katoa shati kaingia kwenye mchezo Mbugi, hawana kanuni, sheria.
CCM ni Mbugi,” alisisitiza Mbowe.
0 Comments