MSAFARA
wa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, juzi
ulikumbana na wakati mgumu baada ya kupokelewa kwa mabango yanayolaani
uamuzi wa serikali ya chama chake kuwaondoa wachimbaji wadogo katika
machimbo ya madini yaliyo jirani na mgodi wa Resolute mjini hapa.
Baadhi ya mabango yalisomeka “Maisha bora yapo ukiwa na uhakika wa
ajira’, ‘CCM oyeeh, nchi yetu ardhi yetu, misitu yetu, mbona
mnatunyanyasa hivyo namba 7’, ‘CCM jibuni kero za wachimbaji wadogo na
tupeni haki zetu tumechoka na ahadi hewa’.
Kutokana na hali hiyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye, alilazimika kuyakusanya mabango yote na kumkabidhi Kinana.
Baada ya kukabidhi mabango hayo, Nape alirejea jukwaani na pasipo
kufafanua zaidi aliwaeleza wananchi waliokusanyika katika Uwanja wa
Pating mjini hapa watambue kuwa mtu anayetoka katika chumba cha mzazi
wao wa kike ndiye baba yao.
Mbali na kauli hiyo, pia Nape alielekeza mashambulizi ya maneno kwa
viongozi wa vyama vya upinzani kwa uamuzi wao wa kuungana pamoja na
kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Kwa upande wake, Kinana kabla ya kumuita Mkuu wa Mkoa wa Tabora,
Fatma Mwasa kujibu kero na mabango hayo, alitoa nafasi kwa mmoja wa
wananchi kuelezea kero hiyo, ambapo kijana aliyejitambulisha kwa jina la
Samson alieleza namna walivyonyanyaswa.
Samson alisema namna zoezi la kuwaondoa wachimbaji wadogo katika eneo
la mgodi wa Resolute ulivyoendeshwa kuna uwezekano mkubwa baadhi ya
watu walifukiwa wakiwa hai kwa kuwa hadi leo hawajulikani walipo.
Alieleza kuwa mwanzoni wachimbaji waliporuhusiwa kuendesha shughuli
zao katika eneo la uchimbaji la namba 7, baadhi yao walikopa mitaji ya
kufanyia kazi ikiwemo kuweka rehani mashamba na nyumba zao.
“Hivi unavyoniona makazi yangu nimeyakimbia kwa madeni, kiwanja
changu nimeshakipoteza na hata baadhi ya jamaa zetu hawajulikani
walipo… tuliambiwa tuondoke katika machimbo katika saa 48, lakini usiku
wa siku tulioambiwa wakaja askari na kupiga mabomu hovyo hovyo, hatujui
kama wengine waliingia kwenye mashimo na kwa kuwa mzungu aliyafukia bila
kushirikisha wananchi huenda ndiyo wamezikwa humo,” alisema Samson.
Katika kujibu kero hizo, Kinana alimuinua Mwasa ambaye badala ya
kujibu alianza kuwafanyia mzaha wananchi kuwa ni mashemeji zake, na
kwamba maswali yao yanaweza kujibiwa na mawifi zake.
“Nisikilizeni mimi shemeji yenu, siyo wale wanaowadanganya na
kuwaambia ‘Peoples Power’, sisi tulikaa na menejimenti ya Resolute
wakasema wataalamu wao watawaonyesheni michoro yenye madini mengi ili
mpate kuchimba,” alisema Mwasa katika majibu yake yaliyozua minong’ono
miongoni mwa wananchi.
Wananchi walizidi kushinikiza kwa sauti awaambie siku maalumu
watakayoanza kuchimba, ambapo Mwasa alisema ameshazungumza na Waziri
Mkuu na kwamba wataruhusiwa na maswali mengine yanapaswa kujibiwa na
wifi zake.
Hali hiyo ilimuinua tena Kinana na kuomba akutane na wawakilishi wa wachimbaji, ili waweze kumuelezea matatizo yao kwa kina.
Kuhusu kero ya maji, Rambo Kabeke alisema mji wa Nzega hauna tatizo
la maji kama inavyodhaniwa bali watendaji wa serikali wamekuwa
wakiendekeza rushwa.
Aliongeza kuwa alishafuatilia huduma hiyo zaidi ya mara tatu bila
mafanikio huku akitakiwa kutoa sh 700,000 ili awekwe katika eneo
lisilokuwa na tatizo la maji.
Katika hatua nyingine ziara hiyo ya Kinana mjini Nzega ilizua mvutano
mkali wa kisiasa baina ya mbunge wa jimbo hilo, Dk. Hamis Kigwangwala
na Katibu wa Fedha na Uchumi wa vijana wa jimbo hilo, Husein Bashe, kwa
kila mmoja kutoa misaada yenye malengo ya kuwaweka karibu na wananchi.
Bashe alikabidhi baiskeli 200, pikipiki nne na kutoa sh milioni tano
katika kuchangia ujenzi wa matawi ya chama, miradi ya mamalishe na ile
ya vijana wanaoendesha bodaboda, huku Dk Kigwangwala akitoa mashine ya
kuangulia kuku na kuahidi kuezeka baadhi ya ofisi za chama.
0 Comments