Baada ya mmoja kati mawaziri wanaotajwa kuwa mizigo, Christopher Chiza, kupata wakati mgumu kupitisha bajeti ya wizara yake ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoundwa na wabunge wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), imepania kukwamisha bajeti ya Wizara ya Maji, inayoongozwa na waziri mwingine mzigo, Profesa Jumanne Maghembe.
Msimamo wa kukwamisha bajeti ya wizara hiyo ulitangazwa jana na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA).
Alisema mwaka wa fedha 2013/14 unaomalizika Julai 30, serikali
iliongeza bajeti ya Wizara ya Maji kufikia sh bilioni 184, lakini fedha
zilizotolewa ni sh bilioni 86 tu na sh bilioni 98 hazijatolewa hadi
sasa, hivyo kukwamisha miradi mingi ya maji nchini.
“Kwa hali hiyo hakuna sababu yoyote ya kujadili bajeti ya maji ya
mwaka 2014/15, kwani bajeti ya mwaka uliopita hajatekelezwa pamoja na
viongozi wa serikali kutumia Bunge kuwadanganya wananchi, kwamba suala
la maji katika maeneo mbalimbali nchini, likiwemo Jiji la Dar es Salaam
litakuwa historia,” alisema Mnyika.
Aliongeza: “Kwa kuwa tayari randama iliwasilishwa mezani na
haikuwafikia wabunge wote kwa wakati, mimi nimeipata na nimeisoma kwa
makini na nimegundua kwamba miradi mingi ya maji haijatekelezwa licha ya
kuwepo mpango mzuri wa vijiji 10 kila wilaya kupatiwa maji, lakini bado
hata miradi hiyo haijatekelezwa hadi sasa.
“Jambo hili ni zito kuliko jambo lolote kwani inaonyesha wazi kuwa
tatizo la maji kwa Watanzania halina ufumbuzi, hivyo hakuna sababu ya
kujadili hotuba hiyo na badala yake inatakiwa irudishwe, ili ipitiwe
upya na kamati na hapo ndipo itaweza kujadiliwa.”
Mnyika alisena anakusudia kumwandikia barua Waziri Magembe, ili
asisome bajeti yake leo kwa madai kuwa miradi mingi ya maji iliyopangwa
katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014 hajatekelezwa na mingine
haijaanza kabisa.
Mbunge huyo ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, alienda
mbali kwa kumtaka Maghembe pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira, kuwajibika kwa kujiuzulu kwa
kutumia Bunge kuwadanganya wananchi juu ya mpango mkubwa wa maji katika
maeneo mengi nchini.
Mnyika alisema kuwa analazimika kufanya hivyo kutokana na bajeti yake
kuwa na mapungufu mengi ambayo hayatoi ufumbuzi kwa Watanzania juu ya
tatizo la maji, hususani katika Jiji la Dar es Salaam.
Mbali na hilo, alisema hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka
huu wa fedha, ina upungufu mkubwa kutokana na kile alichoeleza kuwa ni
uongo wa mawaziri wa wizara hiyo ambao waliwapa matumaini makubwa
Watanzania.
Alisema serikali haina dhamira ya kweli katika kutafuta ufumbuzi wa
tatizo la maji na badala yake wamekuwa wakitumia shida za Watanzania
kufanya siasa ambazo hazina matokeo na mipango ya kimaendeleo.
Kwa mujibu wa Mnyika, kama Waziri Maghembe atalazimisha kuisoma
bajeti hiyo, atamjulisha Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa
ushirikiano wa Baraza la Mawaziri Kivuli la UKAWA, kupanga mikakati ya
kukwamisha bajeti hiyo.
Alisema katika hatua hiyo Waziri Mkuu Mizengo Pinda ndiye analazimika
kutoa hoja ya kuondoa bajeti ya Wizara ya Maji isijadiliwe na
asipofanya hivyo, naye atatakiwa kuchukuliwa hatua kali.
“Suala la maji siyo kwa Jiji la Dar es Salaam tu, ili ni janga la
kitaifa. Hata katika vijiji kumi ambavyo viliingizwa katika mpango wa
matokeo makubwa sasa na badala yake mpango huo umegeuka kwa kasi kuwa
mpango wa matokeo mabaya sasa,” alisema Mnyika.
Wakati wa Bunge la Bajeti la mwaka wa fedha uliopita, Mnyika
aliwasilisha hoja binafsi kuhusu tatizo la maji jijini Dar es Salaam,
lakini ilizimwa bungeni kwa madai kuwa serikali ina mpango wa miradi
mikubwa ya maji kwa nchi nzima.
0 Comments