Watu zaidi ya hamsini na tano wamefariki katika maeneo mbali mbali nchini Kenya baada ya kunywa pombe 'haramu'.
Maeneo hayo yako katika mkoa wa kati na katika eneo la Mashariki mwa Kenya.
Maeneo hayo ni pamoja na majimbo ya Kiambu ambako watu 15 wamefariki, Jimbo la Embu Mashariki mwa nchi ambako wengine zaidi ya 20 wamefariki.
Katika majimbo ya Kitui na Makueni mashariki mwa Kenya watu 20 wameripotiwa kufariki.
Vifo hivyo vilitokea kuanzia Jumapili siku ambayo watu zaidi ya miamoja walibugia pombe haramu inayosemekana ilikuwa imechanganywa na kemikali aina ya Methanol ambayo ni sumu kwa mwili.
Inaarifiwa wengine zaidi ya miamoja wamelazwa hospitalini baada ya kubugia pombe hiyo haramu siku ya Jumapili, baadhi wakiwa katika hali mahututi huku wengine wakiwa wamepoteza uwezo wao wa kuona.
Watu hao inashukiwa walikunywa mvinyo ambao ulikuwa umechanganywa na kemikali ya Methanol.
Mwanamume mmoja ambaye alienda ulevini na mkewe alisema kuwa mke wake alianza kwa kupoteza uwezo wake wa kuona na kisha kufariki muda mfupi baadaye.
Wengi waliofikishwa hospitalini walikuwa wanaumwa na tumbo, wanahisi kisunzi na kuumwa na kichwa. Wengine walifikishwa hospitalini wakiwa katika hali mahututi na kufariki wakipokea matibabu.
Shirika la kupambana na utumiaji wa pombe na madawa ya kulevya, NACADA limesema kuwa wale waliohusika katika uuzaji na usambaji wa pombe hiyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Vita dhidi ya pombe haramu nchini Kenya vimekuwa vigumu kushinda kwani watu wenye kipato cha chini huchagua kutumia pombe ya bei nafuu ambayo huwa sio pombe halali na kukabiliwa na hatari kama hizi.
0 Comments