HILA za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumshambulia aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, huku wakitumia kitisho cha jeshi kuasi iwapo mfumo wa serikali tatu utaridhiwa zimegonga mwamba.
Tangu rasimu ya pili ya katiba inayopendekeza muundo wa serikali tatu
itolewe na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, makada wa CCM
wamekuwa wakimshambulia binafsi Warioba kwa madai hana nia njema na
taifa, ndiyo maana amependekeza mfumo huo.
Rais Jakaya Kikwete, ni miongoni mwa watu waliokuwa mstari wa mbele
kupinga mapendekezo ya rasimu kwa madai kuwa hayatekelezeki, na iwapo
muundo wa serikali tatu ukikubalika, kuna hatari jeshi likapindua
utawala.
Kauli hiyo aliitoa wakati akifungua Bunge Maalumu la Katiba, ambapo
pia alikosoa takwimu za watu waliohojiwa na waliotaka muundo wa serikali
tatu, huku akidai ukipita jeshi litapindua nchi.
Rais Kikwete alisema jeshi litakua hatua hiyo kwakuwa Serikali ya
Muungano ambayo itakuwa na jeshi haitokuwa na vyanzo vya mapato, na
hivyo kukosa fedha za kuwalipa wanajeshi.
Hata hivyo, wiki iliyopita Warioba amejibu mapigo kwa kuwataka
watawala waache kulihusisha jeshi na masuala yao ya kisiasa kwakuwa lina
uzalendo mkubwa kwa Tanzania.
Alibainisha kuwa jeshi limekuwa likifanya kazi wakati nchi ikiwa
kwenye hali ngumu, hususan katika vita ya Kagera na halijapata kuasi
wala kupindua serikali.
Alibainisha kuwa ni hatari sana kwa wanasiasa kutumia jeshi kama
mbinu za kushawishi umma kwa maslahi ya kisiasa ili waendelee kubaki
madarakani.
“Kwa hili ni kama unataka kuchochea kwa kuwa unataka serikali mbili,
sasa wasitishe wananchi kwamba ‘msipokubali serikali mbili jeshi
litachukua madaraka’. Kwa maana nyingine unaliambia jeshi ni baya,
litachukua madaraka. Kuna sababu gani ya kufika hapo?
“Unataka kuchochea jeshi liasi kwa kisingizio kwamba hawalipwi
mishahara, kwanini jeshi lisilipwe na sio mawaziri au watumishi
wengine?” alisema.
Alisema kuwa jeshi haliwezi kupindua utawala kwa sababu ya wananchi
kuamua kuingia kwenye mfumo wa serikali tatu kama inavyonadiwa na
watawala.
Warioba alisema miongoni mwa taasisi zenye uzalendo mkubwa kwa muda
mrefu ni jeshi na limekuwa likifanya kazi zake katika mazingira magumu
bila kulalamika au kudai stahiki zao.
Alisema kama kuasi, jeshi lingefanya hivyo mara baada ya kutoka
katika vita ya Kagera ambapo hali ya kiuchumi ilikuwa mbaya, huku huduma
za msingi zikisuasua. Lakini lilionyesha uzalendo mkubwa.
Alibainisha kuwa uzalendo huo wa jeshi hauwezi kumalizika iwapo taifa
litaingia kwenye mfumo wa serikali tatu kama baadhi ya wanasiasa
wanaeneza vitisho.
Mashambulizi kwa Warioba
Msimamo huo wa Rais Kikwete uliwafanya wajumbe wengi kutoka CCM
kumshambulia Warioba walipokuwa wakichangia sura ya kwanza na sita
katika vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.
Mashambulizi hayo yalifikia hatua ya kugusia maisha binafsi ya
Warioba ambapo Abdallah Bulembo, alisema kiongozi huyo si safi kwakuwa
alifutiwa ubunge wake mwaka 1991 kwa kutoa rushwa ya nyama, mchele na
fedha.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi naye aliingia katika mkumbo wa kumpinga Warioba huku akidai kuwa
muundo wa serikali tatu utakaribisha utawala wa Kiislamu Zanzibar.
Lukuvi, alisema utawala huo ukirejea Zanzibar, waumini wa dini
nyingine hawatokuwa na fursa ya kuabudu kwa uhuru kama wanavyofanya hivi
sasa kwakuwa miongoni mwa wanaotaka serikali tatu ni kikundi cha Uamsho
kinachoshirikiana na Chama cha Wananchi (CUF).
Hata hivyo, wakati CCM ikionekana kujikita kwenye mashambulizi dhidi
ya Warioba, wanayedai ana lengo la kuuvunja muungano, Rais Kikwete
alimpa nishani ya kumbukumbu ya miaka 50 ya muungano daraja la kwanza.
Sababu mojawapo ya kumpa nishani hiyo ni kutokana na kuwa Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeuenzi na bado anauenzi muungano
huo.
“Katika kipindi chako, pamoja na nyadhifa nyingine, ulikuwa Waziri
Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania…katika kipindi hicho na hadi sasa umeendelea kuwa mwaminifu,
umeutunza, umeulinda na umeuenzi muungano,” ilisema sehemu ya taarifa ya
kutoa nishani.
Kitendo cha Warioba kupewa nishani hiyo kimezua gumzo kubwa miongoni
mwa wana CCM ambao wanaona Rais Kikwete kawasaliti kwa kumbeba kada
mwenzao mwenye lengo la kuuvunja muungano.
Hata hivyo, hadi sasa kuna mpasuko mkubwa ndani ya CCM kwakuwa baadhi
ya makada hawaamini katika serikali mbili au kumshambulia Warioba
binafsi au wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kingunge Ngomabare Mwiru, ni miongoni mwa makada wanaopinga
mashambulizi dhidi ya Warioba ambapo alisema watu wanaofanya hivyo
wanakitukanisha chama na hawana adabu.
Warioba awaumbua
Hata hivyo, Warioba amejibu mashambulizi hayo huku akidai watawala
ndio wamemsaliti Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa
kuruhusu uvunjaji wa katiba aliokuwa akiutetea.
Jaji Warioba wiki iliyopita alikemea tabia ya watawala kumtumia
Mwalimu Nyerere kama hirizi wanapotaka kupitisha mambo yao, huku
wakimsaliti kwa matendo yao.
Katika mazungumzo yake kwenye kipindi cha ‘Dakika 45’ cha ITV wiki
iliyopita, Jaji Warioba alisema kamwe hajamsaliti Baba wa Taifa kwa
kuleta mapendekezo ya serikali tatu, bali tume imetazama mapendekezo na
hali halisi ya wakati tuliomo.
Badala yake Jaji Warioba amesema Mwalimu Nyerere hakuwa na mawazo ya
mgando, kwa hiyo wasingemtegea kwamba wakati wote yale aliyokuwa nayo
kama angekuwepo angekuwa na hayo hayo.
“Mwalimu alikuwa anafuata wakati ulivyo, lakini kubwa zaidi hao
wanaosema hivyo ndio wamemsaliti Mwalimu… Nilisema Mwalimu ametuachia
muungano ambao Bunge la Muungano lilikuwa na madaraka kamili,
wameharibu… Mahakama ilikuwa na madaraka kamili wameharibu.
“Aliacha nchi moja, wamezigeuza nchi mbili, wakati wa Mwalimu mizinga
ilikuwa inapigwa kwa rais wa nchi, sasa hivi wanapiga mizinga kwa
marais. Wamevuruga muungano, hawaambiliki wanakimbilia kumgeuza Nyerere
kama hirizi,” alisema.
Jaji Warioba alifafanua kuwa wakati wa Mwalimu mambo 22 ya muungano
yaliyomo kwenye katiba, alipotoka kama rais yalikuwa 21 na lile la 22
kuhusu vyama vya siasa lilikuja baadaye.
“Lakini hata Rais Kikwete alipokwenda kwenye Bunge la Katiba alieleza
kila moja ya mambo yale yaliingiaje kwenye katiba na lini yaliingia.
Yaliingia kikatiba, wao wameyaondoa kinyemela bila kupitia katiba.
“Mwalimu alikuwa analinda katiba, sasa wanasema mimi msaliti… Leo
Mwalimu angetoka akaona haya aliyowatendea, angesema mimi ndiye msaliti
ama wao?” alihoji.
0 Comments