MWENYEKITI
wa Bunge Maalumu la Katiba, na Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
Samuel Sitta, juzi alipata wakati mgumu baada ya kulakiwa na kundi kubwa
la watu, wengi wao wakiwa vijana waliokuwa na mabango yaliyobeba ujumbe
wa ‘serikali tatu’.
Hali hiyo ilijitokeza kabla na baada ya kufungua matawi mawili ya CCM
katika eneo la Sahara jijini hapa, ambapo idadi kubwa ya watu
wanaodaiwa ni wafuasi wa vyama vya upinzani, walipaza sauti zao kila
mara wakimwonyesha alama ya vidole vitatu, wakiashiria kutaka muungano
wa serikali tatu na wengine wakionyesha alama ya vidole viwili
inayotumiwa na CHADEMA.
Awali hali hiyo haikuonekana kumshitua kiongozi huyo, lakini ongezeko
la watu wakati wa ufunguzi wa matawi hayo, waliokuwa wakipaza sauti zao
kutaka maoni ya wananchi waliotaka serikali tatu yaheshimiwe,
kulimtikisa kiasi cha kumfanya akatishe hotuba yake mara kwa mara.
Kila mara makundi ya watu hao, hususan vijana, walikuwa wakikatiza
hotuba yake kwa kuimba; “Tunataka serikali tatu, tunataka serikali tatu,
CCM kwisha, CCM kwisha.”
Baadhi ya vijana wa UVCCM, walionekana kukerwa na hali hiyo, ambapo
nao walianza kupaza sauti zao wakimshangilia Waziri Sitta kwa kumuita
“Jembe, jembe, jembe, jembe.”
Waziri Sitta, alikuwa amepiga kambi jijini Mwanza kwa siku mbili
kukutana na kuzungumza na makundi mbalimbali ya vijana wajasiriamali, na
kufungua matawi hayo mawili na kituo cha Thamani ya Utu kilichopo
kwenye kituo cha mafuta cha MOIL Sabasaba, Manispaa ya Ilemela jijini
hapa.
Sitta, aligusia kidogo suala la katiba, akitaka izibane idara zote za
umma na kuwa rafiki wa wananchi, kuliko ilivyo sasa ambapo viongozi
wengi wanaonekana kuvimba vichwa wanapokuwa kwenye ofisi zenye viyoyozi.
Akizungumza mara baada ya kufungua tawi la CCM la wapiga debe stendi
ya daladala Sahara, Waziri Sitta alisisitiza umuhimu wa viongozi wa
idara zote za serikali wakiwemo maofisa uchumi wa kila halmashauri
nchini, kushirikiana na vijana kuwawezesha mbinu na maarifa ya kubuni na
kusimamia miradi ya kimaendeleo.
Alisema vijana ndio nguzo muhimu sana katika maendeleo ya taifa,
hivyo ni lazima suala hilo litiliwe mkazo kwani Tanzania ilipata uhuru
wake kwa ajili ya kuwakomboa wananchi wake kutoka kwenye makucha ya
wakoloni, ili wajitawale na kupigania maendeleo yao.
“Nikiwa Waziri wa Afrika Mashariki, nimepanga kuhakikisha vijana wa
Mwanza ninawaunganisha na vijana wa Kigali Rwanda, Nairobi Kenya,
Kampala Uganda na miji mingine ya Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki, ili
waweze kujitanua kimaendeleo kupitia miradi yao.
“Kumbukeni hapa Mwanza ndiyo kitovu cha nchi za Maziwa Makuu, kwa
hiyo tunahitaji kuona vijana mnajinasua kutoka kwenye lindi la
umasikini. Na leo hapa nayakabidhi mashina haya mawili ya CCM
niliyoyafungua sh 500,000 kila moja,” alisema Waziri Sitta huku
akishangiliwa.
Alisema ziara yake hiyo ililenga kukamilisha ratiba yake ya mwaka
2013 iliyohusu kukutana na kuzungumza na makundi mbalimbali ya
wajasiriamali, na kuonya kuwa taifa lolote linalowapuuza vijana lina
matatizo makubwa.
0 Comments