MSHAMBULIAJI mkongwe wa
kimataifa wa Ujerumani, Miroslav Klose ambaye ameweka rekodi akiwa na
timu ya taifa ya nchi hiyo kwa kushinda michuano ya Kombe la Dunia mwezi
uliopita amestaafu rasmi soka la kimataifa. Klose ambaye amefunga mabao
mawili katika michuano hiyo iliyofanyika nchini Brazil ameweka rekodi
ya kufunga mabao mengi zaidi katika kwa kufikisha mabao 16. Klose
amesema katika taarifa aliyotoa kuwa kushinda Kombe la Dunia nchini
Brazil ilikuwa ni ndoto zake toka akiwa mdogo. Nyota huyo mwenye umri wa
miaka 36 aliendelea kuwa ana furaha na anajivunia kutoa mchango mkubwa
katika soka la Ujerumani kwa kipindi cha miaka 13 aliyoitumikia na
anadhani huo ni wakati muafaka wa kufunga ukurasa huo. Klose ambaye ni
mchezaji wa pili kucheza mechi nyingi zaidi kwa Ujerumani akiwa amecheza
mechi 137 alianza kuitumikia nchi hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 2001 na
kuja kuwa mfungaji bora akifunga mabao 71 na kuipita rekodi ya miaka 40
ya Gerd Mueller aliyefunga mabao 68.
0 Comments