Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema
zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura linalotarajiwa kuanza
hivi karibuni linamhusu kila raia mwenye sifa ya kupiga kura.
Ufafanuzi huu unakuja wakati pakiwa
na mawazo tofauti ya nani hasa anatakiwa kushiriki katika zoezi hilo huku
baadhi ya watu wakidhani kuwa jambo hili linawahusu wale ambao hawakupata
kujiandikisha kupiga kura au waliopoteza kadi au waliofikia umri wa kupiga
kura.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu,
Damian Lubuva amesema jana jijini Dar es Salaam kuwa katika kufanya maboresho
hayo na kupata daftari linaloaminika zaidi, Tume inatarajia kutumia mfumo mpya
wa “Biometric Voters Registration System” au mfumo ambao utatumia utambuzi wa
watu kwa alama za binadamu.
Kwa kutumia mfumo huu, muhusika
atachukuliwa alama za vidole vyote vya mikono 10, picha na sahihi yake.
Hii ni tofauti na mfumo uliokuwa
unatumika wa “Optical Mark Recognition” (OMR) ambapo muhusika alikuwa anajaza
fomu na kuchukuliwa alama ya kidole kimoja tu ambapo Jaji Lubuva anasema ulikuwa
na uwezekano wa watu kujiandikisha hata mara mbili bila kutambulika.
“Watu wote wenye sifa watatakiwa kujiandikisha
upya katika mfumo huu mpya na kupatiwa kadi mpya,” alisema.
Akitoa ufafanuzi zaidi alisema uboreshaji
wa daftari hilo unatokana na matakwa ya kisheria na malalamiko ya wadau
mbalimbali.
Alisema tangu kufanyika kwa uchuguzi
mkuu mwaka 2010 pamekuwa na malalamiko toka kwa wadau mbalimbali kama vyama vya
siasa, mashirika yasiyo ya kiserikali na wapiga kura wenyewe kuhusu haja ya
kuboresha daftari hilo na kuondoa watu ambao hawastahili kuwamo kama
waliofariki na kuongeza wengine wenye sifa.
“Malalamiko haya yanafanya imani ya
watu juu ya daftari la wapiga kura iwe ndogo,” alisema.
Alifafanua kuwa sheria inaitaka NEC
kuboresha daftari la wapiga kura mara mbili kati ya uchaguzi uliopita na
uchaguzi unaokuja.
“Ni kutokana na matakwa ya kikatiba
na sheria na malalamiko haya, NEC imelazimika kufanya zoezi hili kabla ya kura
ya maoni na uchaguzi mkuu ujao 2015,” alisema.
Akizungumzia matayarisho ya zoezi
hilo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bw. Julius Mallaba alisema yanaridhisha na
kuendelea vizuri.
Alisema maboresho ya daftari hilo kwa
awamu hii ni mahsusi kwa ajili ya kura ya maoni kuhusu katiba mpya mapema mwaka
2015, uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 pamoja na chaguzi ndogo zitakazofuata baada
ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Sehemu kubwa ya maandalizi ya
uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura yamekamilika,” alisema.
Akielezea zaidi Bw. Mallaba alisema
tayari NEC imeanzisha na kuhakiki vituo vipya na kuviweka katika ngazi ya
vitongoji, vijiji na mitaa.
Vituo hivyo vimeongezeka kutoka vituo
vya awali 24,919 na kufikia vituo 40,015 nchi nzima.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa tayari
ununuzi wa vifaa vya uandikishaji ikiwemo Biometric Voter Registration Kits
umeshafanyika.
“Maandalizi ya melekezo kwa maafisa
waandikishaji, waandishi wasaidizi pamoja na vyama vya siasa yameshafanyika,”
alisema na kuongeza kuwa kanuni za uboreshaji zimeshaandaliwa.
Alisema kuwa maandalizi ya kituo cha
kuhifadhia taarifa na mkakati wa utoaji wa elimu ya mpiga kura na machapisho
mbalimbali tayari yameshakamilika.
Aliongeza kuwa katika maandalizi
hayo, Tume imeshakutana na wadau mbalimbali kama wahariri, viongozi wa dini na
vyama vya siasa ili kujadiliana na kupata maoni yao kuhusiana na zoezi hilo.
“Tunashukuru sana kwa michango ya
mawazo yao…tunayapokea na kuyafanyia kazi,” alisema na kuongeza kuwa katika
kuboresha zaidi, Tume inatarajia kukutana na makundi mengine kama vijana, kina
mama na walemavu.
NEC imepewa jukumu la kisheria
kuandikisha wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura na kuliboresha
daftari hilo kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na wabunge ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
0 Comments