Katika
kuunga mkono jitihada za serikali kubaini aina mbalimbali za vivutio
vya utalii mkoani Njombe, shirika lisilo la kiserikali la SUMASESU
lililopo wilayani Makete mkoani hapo limeunga mkono jitihada hizo kwa
kubaini mlima Ihobwela uliopo kata ya Tandala kuwa ni miongoni mwa
vivutio vya utalii wilayani hapo
Aidha
watumishi 16 wa shirika hilo wakiambatana na wageni 15 kutoka Ujerumani
wamepanda mlima huo hivi karibuni na kubaini kuwa mlima huo unapaswa
kuingizwa katika vivutio vipya vya utalii wilaya ya Makete kutokana na
muundo wake pamoja na miti ya asili iliyopo katika mlima huo
Akizungumza
na mwandishi wetu mara baada ya kupanda na kushuka salama katika mlima
huo, Mkurugenzi wa shirika la SUMASESU Bw. Egnatio Mtawa amesema mlima
huo una vilele vitatu tofauti vyenye mawe ya kuvutia pamoja na aina
mbalimbali za mimea ya asili
Amesema
ameamua kupanda mlima huo na watumishi wenzake pamoja na wageni
waliowatembelea kutoka Ujerumani, ili kuona ni jinsi gani wilaya hiyo
imejaa vivutio mbalimbali huku akisema kuwa ukiwa kwenye vilele vya
mlima huo unaweza kuona vijiji mbalimbali vya wilaya ya Makete pamoja na
Ziwa Nyasa
"Wilaya
ya Makete ina vivutio vingi, mimi nitoe wito tu kwa jamii kuendelea
kugundua na kuvibainisha vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo
wilayani mwetu, ili serikali ivitambue na kuhakikisha vitaendelea kudumu
na kuingiza kipato kwa wilaya na taifa kwa ujumla" amesema Mtawa
Amesema
kuwa miongoni mwa wageni hao kutoka Ujerumani waliopanda mlima huo wapo
walemavu wa aina mbalimbali ikiwemo ulemavu wa akili kwa viwango
tofauti, lakini wameonesha ujasiri wa hali ya juu kwa kupanda mlima huo
na kushuka wakiwa salama
"Mimi
ni mara yangu ya kwanza kupanda mlima huu, mwanzoni nilikuwa nauona tu
nikipita barabarani na kwa muonekano wake nilidhani ni vigumu ulivyo kaa
mtu kuweza kupanda, na pia sikujua kama una vilele vitatu, mi nilijua
kipo kilele kimoja tu, nawashauri wanamakete waje waupande huu mlima
wajionee mandhari nzuri na uumbaji wa MUNGU ulivyo" amesema Mwaija
Kisingile ambaye alifanikiwa kuupanda mlima huo
Mlima
Ihobwela upo katika kata ya Tandala wilayani Makete na una vilele
vitatu vyenye sifa tofauti tofauti na inapendekezwa na wadau hao
serikali iangalie namna ya kuufanya kuwa vivutio vipya vya utalii na
wananchi wanaouzunguka kuhakikisha wanatunza mazingira yake ili uendelee
kuwepo
Na Edwin Moshi, Makete
0 Comments