Advertisement

Responsive Advertisement

WANAFUNZI WA LUPALILO SEKONDARI WASHAURIWA KUEPUKA KUJIHUSISHA NA VITENDO VYA NGONO


Na Edwin Moshi, Makete.
Wanafunzi wilayani Makete mkoani Njombe wameshauriwa kujiepusha na vitendo vinavyoweza kusababisha wasifikie malengo yao ikiwemo kujihusisha na mapenzi. 
Hayo yamesemwa na Bi Anifa Mwakitalima na Bw. Faustine Mwenda kutoka shirika lisilo la kiserikali la SUMASESU wakati wakitoa elimu ya ujana kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Lupalilo iliyopo kata ya Tandala wilayani hapo. 
Bi. Mwakitalima amesema kumekuwepo na vitu vinavyochangia wanafunzi hao wasifikie malengo yao ikiwemo kujihusisha na mapenzi ili hali wao ni wanafunzi na wengi wao wameishia kupata ujauzito na magonjwa ya ngono ikiwemo UKIMWI. 
Amesema misimamo yao itasaidia wao kufikia malengo yao kwa kuhakikisha wanasoma kwa bidii wakifahamu kuwa suala la mapenzi lina muda wake na endapo watajihusisha na masomo watafaulu na kupata kazi nzuri na ndipo wajiingize katika mapenzi kwani muda utakuwa umefika.
Kwa upande wake Faustine Mwenda amewataka wanafunzi hao kuwa makini na wanaowarubuni kimapenzi na kuwataka kuwa na uthubutu wa kukataa na kutoa taarifa pindi wanapokutana na changamoto hizo ili wasaidiwe. 
Mwenda amesema wao kama SUMASESU wanatamua umuhimu wa wanafunzi kufikia malengo yao kwani litapatikana taifa lenye wasomi wazuri na wanaojitambua lakini hayo hayawezi kuja bila jitihada zao za kupambana na vitendo vyote vitakavyosababisha wasifikie malengo yao. 
Shule ya sekondari Lupalilo ni miongoni mwa sekondari kongwe wilayani hapo na yenye wanafunzi wengi hasa wa kike ambapo elimu kama hizo zimekuwa zikitolewa kwao kuwasaidia kuepukana na vishawishi vinavyowasababisha wasifikie malengo yao, ambapo wengi wao wamekuwa wakizitumia stadi hizo na kufaulu vizuri kielimu

Post a Comment

0 Comments