Rais
Jakaya Kikwete ameelezea huzuni na masikitiko yake makubwa kufuatia
vifo vya watu 39 vilivyotokea katika ajali ya barabarani wilayani
Butiama, Mkoa wa Mara, ambako pia watu 79 wameumia, baadhi yao vibaya.
Mara
baada ya kupata taarifa hiyo iliyotokea juzi asubuhi, Rais Kikwete
ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Arusha, amemtumia
salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mara, akielezea huzuni na
masikitiko yake.
“Nakuomba
uwafikishie wafiwa wote pole zangu nyingi sana, ukiwajulisha kuwa niko
nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Aidha, napenda uwajulishe
kuwa naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu aziweke pema roho za
marehemu.”
Kufikia
jana, Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Phillip Kalinji alisema hakuna
watu zaidi waliopoteza maisha. Aidha, alisema wote waliokufa, isipokuwa
wawili tu, miili yao imetambuliwa na ndugu zao.
Hata
hivyo, alisema hakuwa katika nafasi nzuri ya kuwataja marehemu na
majeruhi wa ajali iliyohusisha magari matatu, yakiwemo mabasi
yaliyogongana uso kwa uso na gari dogo aina ya Nissan Teranno
lililogongwa na kutumbukia mtoni.
Mabasi
yaliyogongana juzi majira ya saa 5:30 asubuhi ni Scania lenye namba za
usajili T 736 AWJ mali ya Kampuni ya Mwanza Coach lililokuwa linatokea
Musoma kwenda Mwanza na lingine aina ya Zoutong, lenye namba za usajili T
677 CYC mali ya Kampuni ya J4 Express lililokuwa linatokea Mwanza
kwenda Musoma. Gari dogo lililogongwa aina ya Nissan Terrano lina namba
za usajili T 332 AKK.
Mwandishi
alifanikiwa kuwafahamu waliokufa kuwa ni daktari wa Hospitali ya Mkoa
wa Mara, Dk Anatoria Ntangeki na Sayi Hassan aliyekuwa Mhandishi wa
Mradi wa Umwagiliaji mkoani Mara.