Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana kilianza mkutano mkuu wa chama hicho ambapo Baraza la Wazee wa chama hicho lilichagua viongozi wake.
Akifungua
mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza hilo anayemaliza muda wake, Nyangaki
Shilungushela aliwataka wazee kushikamana na kusaidia ujenzi wa taifa
kwani wazee ni hazina ya busara.
Alisema
kupitia mkutano huo ambao pia unachagua viongozi wapya wa baraza hilo,
aliwataka wajumbe kuchagua kwa haki na wasifuate mkumbo kwani chama
kinahitaji wazee wenye uwezo wa kusaidia ujenzi wa taifa.
Awali
akitoa salamu za chama hicho, Katibu Mkuu wa Chadema Willbrod Slaa
aliwapongeza wajumbe wa baraza hilo kwa kuitikia mwito wa kushiriki
kwenye mkutano huo.
Slaa
aliwashauri kuwa ni vyema kuchagua viongozi kwa uhuru na kamwe
wasikubali kurubuniwa kwa kupewa rushwa, kwani kufanya hivyo
kutasababisha kupatikana kwa viongozi wa wazee wasioweza kusaidia taifa
wala chama.
Mkutano wa chama hicho unaendelea leo na utamalizika Septemba 16, mwaka huu.