Na Ojuku Ibrahim MAAZIMIO ya
Mkutano Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya kuitisha
maandamano na migomo isiyokoma nchi nzima kupinga kuendelea kwa vikao
vya Bunge Maalum la Katiba (BMK) na baadaye kauli kali ya Jeshi la
Polisi ya kukataza kitendo hicho na kutishia kutumia nguvu kuyazima,
yanaweza kusababisha maafa kama busara hazitatumika kwa pande zote
mbili.
Hayo yamesemwa na baadhi ya wananchi wa kada na vyama mbalimbali
waliohojiwa kufuatia kuitwa polisi na kuhojiwa kwa Mwenyekiti wa Chadema
Freeman Mbowe aliyetoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa chama hicho hivi
karibuni.
Chacha Maiya, aliyejitambulisha kama mwanafunzi wa sheria kutoka Chuo
Kikuu Huria, alisema ingawa ni haki ya msingi kwa wananchi kuandamana,
lakini tafsiri inayotokana na maneno ya Mbowe ni kama inayoashiria
vurugu kutoka kwa wafuasi wake, jambo ambalo halikubaliki.
“Ni kama vile Mwenyekiti Mbowe anawahamasisha wafuasi wake kufanya
vurugu. Nadhani kulikuwa na haja ya kuwa makini katika kutoa matamshi
hasa unapotaka kuhamasisha umma, sasa suala la msingi ni kwa wao
kusitisha maandamano yao na kufikiria njia nyingine ya kuwasilisha
ujumbe wao kwa Rais au Bunge,” alisema.
Akizungumzia sakata hilo, kiongozi mmoja wa Chadema aliyeomba hifadhi
ya jina lake, alisema kitendo cha polisi kuzuia maandamano yao hakiwezi
kulipa uhalali Bunge Maalum kuendelea, isipokuwa wanazidi kuchochea ari
ya wananchi katika kutafuta haki yao.
“Ipo siku watu watasema basi, imetosha, hivi vitisho vina mwisho
wake, polisi wanataka kuingilia siasa kwa kuilinda CCM, lakini watambue
kuwa hakuna sheria inayowapa mamlaka ya kuzuia maandamano ya kisiasa,
walichopaswa kufanya, ni kutoa maelekezo ya namna ya kufanikisha
maandamano hayo ili yatawaliwe na amani, siyo kupiga watu mabomu,”
alisema.
Tokea kutolewa kwa maazimio hayo ya Chadema, wafuasi kadhaa wa chama
hicho wamekamatwa katika maeneo mbalimbali nchini na wengine kufikishwa
mahakamani, baada ya kujaribu kuandamana na polisi kutumia nguvu
kuwazuia.
0 Comments