Advertisement

Responsive Advertisement

Katiba mpya hisia tofauti


RASIMU ya tatu ambayo imetolewa hadharani juzi na Bunge Maalum la Katiba, imepokewa kwa maoni mbalimbali. Baadhi ya wananchi wameipongeza kwa kuingiza mambo ya msingi na wengine wameonesha kutoridhishwa na rasimu hiyo.


Wakizungumza na gazeti hili jana, baadhi ya wasomi, viongozi wa dini na watendaji wengine wa taasisi mbalimbali, walisema yapo mambo ambayo yamefuata kilio cha muda mrefu cha wananchi wengi kama suala la mgombea binafsi.

Lakini, wengine wamesikitishwa na baadhi ya maoni ya wananchi kutupwa, kama la mawaziri kuteuliwa kutoka miongoni mwa wabunge.

Mgombea binafsi Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisifu rasimu kuwa na mgombea binafsi na kuwa hicho ndicho kilio cha muda mrefu cha wananchi, ambao wangependa kuwa na kiongozi asiyefungamana na upande wowote.

Alisema rasimu hiyo inatoa mwanya kwa watu binafsi, waliokuwa wanatamani kuwania nafasi yoyote bila ya kushiriki kupitia kwenye chama cha siasa.

“Sasa naamini watajitokeza wagombea waliokuwa na kiu ya kuwania kupitia nyanja nyingine na sio siasa, hivyo tunaweza kupata viongozi wasiotokana na vyama na tukafanya vizuri,” alisema.
Kwa upande wake, Profesa Mkumbo Kitila wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema amefurahishwa na rasimu hiyo kuzingatia mambo muhimu kama vile suala la mgombea binafsi na masuala ya msingi kama vile ardhi.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Method Kilaini amezungumzia rasimu hiyo na kupongeza baadhi ya vipengele, ikiwemo kuwepo kwa mgombea binafsi na Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais.

Makamu watatu wa Rais Katika eneo hili, Dk Bana alisema wananchi wasiogope mfumo huo, kwani hakuna kilichobadilika kwenye mfumo wa uongozi, bali ni majina tu yamebadilika ili kukazia muungano.

Kwa upande wa Muundo wa Muungano, Dk Bana alisema uamuzi uliofanywa wa kuacha muundo wa muungano, kupigiwa kura ya maoni na wananchi wa pande zote, ni jambo zuri, ambalo ndilo lililokuwa kilio cha watanzania wengi, ambao wanataka kuamua muundo wa muungano.

Hata hivyo, alisema yapo mambo ambayo hayakuangaliwa kwa umakini, kama vile nafasi ya Tume ya Utumishi wa Umma.

Alisema katika hilo tume hiyo, haikupewa nafasi kama jinsi tume nyingine mfano ya Mahakama na Bunge ilivyopewa nafasi ya kupata watendaji wake na wajumbe wake na kwamba kwa tume ya utumishi, ambayo ndiyo chombo kikuu cha watendaji wa umma, haikuzingatiwa ipasavyo.

Alisema rasimu ya pili ya Warioba, ilipendekeza kwenye Ibara ya 109, uwepo wa majina matatu yatakayopendekezwa na tume kwenda kwa rais kwa ajili ya uteuzi wa nafasi husika, lakini ibara hiyo imefutwa.

“Nimeshangaa kwa nini ibara hii imefutwa, Tume ya Utumishi wa Umma ni kitu nyeti ambacho waombaji nafasi za uongozi wa juu wangetuma maombi kwenye tume na tume kuchagua wenye sifa na kisha majina matatu kupelekwa kwa rais kwa ajili ya uteuzi, ila nashangaa kimefutwa”, alisema Dk Bana.

Alisema tume ya Mahakama na Bunge zenyewe zimepewa nafasi hiyo na kwamba kufanya hivyo ni jambo muhimu, ambalo linafanya kupatikana kwa viongozi wenye sifa, lakini jambo hilo halikuzingatiwa kwenye tume hiyo ya umma ambayo ndiyo tume mama ya ajira za watendaji serikalini.

Kwa upande wake, Profesa Kitila katika masuala ya muungano na Makamu wa Rais, alisema Rasimu ya Bunge imefunguka zaidi kwa upande wa Zanzibar, ambapo mambo ya msingi yamezingatiwa, ikiwemo suala la muundo wa muungano, mambo ya muungano kupunguzwa kuwa 14 badala ya 21. Profesa Kitila alisema suala la makamu wa rais kuwa watatu, lina mkanganyiko kidogo hasa kwenye kipengele cha mgombea mwenza.

“Ukitafakari kwa umakini utaona ni kwamba suala la serikali tatu halikwepeki, ndiyo maana ya uwepo wa hizo nafasi tatu za makamu wa rais, hicho kipengele cha mgombea mwenza hakina mantiki”, alisema Profesa Kitila.

Hata hivyo, alisema Tume ya Jaji Joseph Warioba ilipendekeza mabadiliko makubwa, kama yalivyokuwa kwenye rasimu ya pili ya katiba mpya na kwamba rasimu hii ya tatu iliyowasilishwa na bunge juzi, imekuja na maamuzi ya kawaida.

Post a Comment

0 Comments