Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Dk Margaret Chan
Wakati
imethibitishwa kwamba katika kila sekunde 40 mtu mmoja duniani huamua
kukatisha maisha yake kwa sababu ambazo zinaweza kuzuilika, Tanzania
imeelezwa kuwa ya nane katika orodha ya nchi zinazoongoza kwa watu wake
kujiua.
Ingawa Jeshi la Polisi
nchini lilipotakiwa kuzungumzia suala hilo lilionekana kuchukua mlolongo
mrefu, utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO), umesema
tabia ya watu kuficha takwimu na kufuatilia matukio ya vifo
inachelewesha uchukuaji hatua wa kudhibiti tabia hiyo ya kujiua.
Msemaji wa Jeshi la
Polisi, Advera Bukumbi juzi alipotakiwa kuthibitisha kwa takwimu
kuhusiana na utafiti huo wa WHO, sababu za kujiua na hata mikoa
inayoongoza kwa matukio ya aina hiyo nchini, alitaka mwandishi wa habari
hizi kumtumia maswali ili yafanyiwe kazi kuanzia wiki ijayo.
Utafiti uliofanywa na WHO
na kutolewa kama Taarifa na Umoja wa Mataifa juzi, unaonesha kwamba
tatizo la kujiua halitiliwi maanani wala kujadiliwa kutokana na
kunyanyapaliwa na kuwepo kwa imani potofu zinazohusishwa na vifo hivyo.
Katika utafiti uliotolewa
wiki tatu baada ya mmoja wa wakali wa Hollywood Robin Williams kujiua,
pia waandishi wa habari wameonywa dhidi ya kuelezea kinagaubaga vifo
hivyo kutokana na hatari ya watu wengine kunakili tabia na maamuzi hayo
kwa jinsi yalivyoelezwa na vyombo vya habari.
WHO, ambayo imesema
kwamba kujitwalia maisha binafsi ni tatizo kubwa la kiafya duniani kwa
sasa linalohitaji hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi yake imetoa taarifa
hiyo baada ya kufanya uchunguzi katika nchi 172 duniani.
Imesema katika mwaka 2012
nchi zenye kipato kikubwa ziliongoza kwa mauaji ya aina hiyo ikiwa na
vifo asilimia 12.7 kwa kila watu 100,000 huku nchi za kipato cha chini
na kati zikiwa ni asilimia 11.2 kwa kila watu 100,000.
Lakini kutokana na nchi
za kipato cha chini na kati kuwa na wingi wa watu, wao ndio waliochukua
nafasi kubwa ya vifo hivyo, kwani robo tatu ya matukio kwa wastani yapo
katika nchi hizo.
Hata hivyo, nchi za
Kusini Mashariki mwa Asia zikiwemo Korea Kaskazini, India, Indonesia na
Nepal ndizo zimefanya theluthi moja ya waliojiua duniani.
Vifo vya kujiua katika
nchi tajiri vinaelezwa kuwa wastani wa robo ya vifo vinavyotokea duniani
kote vya aina hiyo. Aidha utafiti huo umeonesha kwamba njia kubwa
inayotumika karibu duniani kote ni kutumia sumu za mashambani,
kujinyonga, kujipiga risasi na kuruka kutoka katika majengo marefu tabia
ambayo ipo zaidi katika nchi za Asia, hasa maeneo ya miji.
“Kila kifo cha kujiua
huleta huzuni. Inakadiriwa kwamba watu zaidi ya laki nane hufa kwa
kujiua. Lakini pia wapo watu wengi wanaojaribu kujiua kwa namna
tofauti,” alisema Mtendaji wa WHO, Dk Margaret Chan akihitimisha miaka
kumi ya utafiti wa tatizo hilo.
Alisema kwamba athari
inayopatikana kwa familia, marafiki na jamii ni kubwa hata kama watu hao
wanakuwa wamejiua wenyewe. Afya ya akili WHO wamesema takwimu za watu
wanaojiua hazipo sawa kutokana na nchi nyingi kutokuwa na tabia ya
kuweka takwimu hizo.
Kutokana na upungufu huo,
walilazimika kufanya kazi ya ziada ili kuweza kupata wastani wa watu
wanaojiua nchi kwa nchi. Wastani wa dunia wa watu kujiua upo kwa watu
11.4 kwa kila watu 100,000 huku wanaume kama wanawake kwa idadi sawa
wakijaribu kujiua.
Nchi ambazo zinaongoza
kwa vifo vya kujiua ni Guyana (asilimia 44.2 kwa kila watu 100,000),
ikifuatiwa na Korea Kaskazini na Korea Kusini (asilimia 38.5 na 28.9 kwa
kila 100,000).
Nchi nyingine ni Sri
Lanka (28.8), Lithuania (28.2), Suriname (27.8), Msumbiji (27.4), Nepal
na Tanzania (24.9 kila mmoja), Burundi (23.1), India (21.1) na Afrika
Kusini (19.8). Nchi nyingine ni za Russia na Uganda (zote zikiwa na
wastani wa 19.5), Hungary (19.1), Japan (18.5) na Belarus (18.3).
Katika nchi zenye kipato
kikubwa matatizo ya afya ya akili kama msongo wa mawazo umeelezwa
kusababisha asilimia 90 ya vifo vya kujiua ukilinganisha na asilimia 60
katika nchi za Asia kama China na India, WHO imesema.
Shirika hilo la Umoja wa
Mataifa limesema kwamba ni lengo ifikapo mwaka 2020 kuhakikisha kwamba
wanapunguza wastani wa kujiua kwa asilimia 10.
Hata hivyo, utafiti
umeonesha kuna changamoto kubwa kutokana na vifo hivyo kutokea katika
makundi ambayo yanaonekana kutengwa, wengi wao wakiwa masikini, wenye
matatizo mbalimbali na wanaoishi katika hali ya kutothaminiwa au
kukubalika katika jamii.
Magonjwa ya kuambukiza
Utafiti umeonesha kwamba nchi zenye pato dogo ambazo zinahangaika
kuwatimizia wananchi wake mahitaji muhimu yakiwemo ya afya, kukabiliana
na magonjwa ya kuambukiza wana wakati mgumu wa kutambua na kuwasaidia
watu wanaotaka kujiua.
Dk Chan anaamini kwamba
vifo vya aina hii (vya kujiua) vinaweza kuzuiwa. Ametaka nchi mbalimbali
kuendelea na kazi ya kuzuia vifo vya kujiua na hata nchi ambazo hazina
watu wanaojiua zifanye juhudi ya kuhakikisha kwamba zinazuia kutokea kwa
vifo hivyo kwa kuwa wazi kujadiliana na kuweka katika ajenda.
Hata hivyo wataalamu
wamekuwa wakishutumu vyombo vya habari na vile vya kijamii kwa kuelezea
jamii kinagaubaga vifo hivyo hali ambayo inaweza kutumiwa na watu
wengine kujiua.
“Kuna kutowajibika kwa
vyombo vya habari katika suala hili, wanaandika tu, wanakuwa chachu,
habari zao huchochea vifo zaidi,” inasema taarifa hiyo huku ikisisitiza
kwamba namna zinavyoandikwa ni kama vile kuremba aina hiyo ya kufa na
kuiona kwamba ni hali ya kawaida.
Akizungumzia utafiti huo
katika mahojiano na gazeti hili, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na
Watoto, Sophia Simba alisema ni jukumu la wizara yake kuhakikisha amani
katika familia inadumishwa.
Alisema kujiua ni kosa la
jinai na pia ni dhambi, hivyo wizara yake inahamasisha upendo ndani ya
familia kuwepo na mazungumzo ili kuepuka matatizo yanayosababisha watu
kujiua.
“Jamii itambue ni vizuri
kuongea ndani ya familia tangu watu wakiwa wadogo ili inapoonekana
dalili ya tatizo lipatiwe ufumbuzi na sisi kama wizara, kazi yetu ni
kuhamasisha familia kuishi kwa upendo na mawasiliano ya mara kwa mara,”
alisema Waziri Simba.
via>>Habarileo