Mtuhumiwa
Geofrey Kilangwa ‘Simbaiwe’( katikati) aliyetuhumiwa kumuua mwanaye
mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili, Regina Geofrey.
YULE mtoto wa umri wa mwaka mmoja na miezi miwili,
Regina Geofrey aliyeuawa kikatili kwa kunyongwa kisha kuzikwa na mtuhumiwa akiwa ni baba
yake mzazi, Geofrey Kilangwa ‘Simbaiwe’ (27) kwa kuwa alizaliwa akiwa
ametanguliza makalio yake, amezidi kuibua maswali.
Baadhi ya wakazi wa Katavi waliozungumza nasi
walihoji uhalali wa baba kumjadili mtoto katika kuzaliwa kwa sababu ya
kutanguliza kiungo fulani.
Wengine walitaka kujua ni kwa nini kama kumuua mtoto wake, mzazi huyo alisubiri kwa mwaka mmoja na miezi miwili?
Mtuhumiwa ambaye pia ni mganga wa kienyeji anayeishi Kitongoji cha
Mwikang’ombe, Kijiji cha Katuma wilayani Mpanda, alitenda unyama huo
kwa madai kuwa mtoto huyo alizaliwa akiwa ametanguliza makalio, hivyo ni
nuksi kubwa katika shughuli zake za uganga wa kienyeji, madai
yaliyopingwa na watu mbalimbali, zikiwemo taasisi za kutetea haki za
binadamu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, akizungumza
na waandishi wa habari mjini hapa, alidai mzazi huyo alitenda uhalifu
huo Agosti 20, mwaka huu ambapo alikamatwa na Jeshi la Polisi, Agosti
26.
Ilidaiwa siku hiyo ya tukio, mtuhumiwa huyo baada ya kumnyonga
hadi kufa binti yake, alimzika kwa siri katika kibanda chake
anachofanyia shughuli za uganga.
Kamanda Kidavashari alisema mtoto Regina alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa ambao haukufahamika kwa zaidi ya mwezi mmoja.
“Ndipo baba mzazi wa binti huyo alipomchukua marehemu na kwenda
kumuuguza kwa siri pasipo mama yake mzazi kufahamu kwani alimdanganya
kuwa mtoto wao amepelekwa kutibiwa na babu yake mkoani Mwanza,” alisema
Kidavashari.
Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, wakazi wa kitongoji hicho
wakiongozwa na mwenyekiti wao, walimtilia shaka mtuhumiwa kutokana na
tetesi zilizosambaa kwamba, Regina aliuawa na baba yake mzazi na kuzikwa
kwa siri.
Mwenyekiti huyo na wakazi wa eneo hilo walifika nyumbani kwa
mtuhumiwa na kuhoji alipo binti yake, aliposhindwa kujibu wakasema
wampekue ambapo alipinga vikali lakini alipopekuliwa kibandani kwake
walibaini kuwepo kwa tuta dogo lililokuwa limechimbwa siku za karibuni.
Wakazi hao walifukua tuta hilo na kukuta kichwa cha mtoto Regina na ndipo wakalitaarifu jeshi la polisi.
Mama wa marehemu, Maria Exavery (22) alisema hakupewa taarifa kwamba binti yake amekufa.
“Mimi nilikuwa nafahamu Regina yuko kwa babu yake Mwanza akitibiwa,” alisema huku akimwaga machozi.
Naye Regina Kaboni (40), mkazi wa Isamilo Mwanza ambaye alikuwa
akitibiwa na mtuhumiwa, anadai kuwa alishirikishwa katika maziko ya
binti huyo baada ya kufa.“Hata hivyo, nilishtushwa sana kwa kitendo cha
mtuhumiwa kumzika mwanaye bila mkewe, nilipomuuliza akadai mila za
kwao mtoto aliyezaliwa kwa kutanguliza makalio, mama mzazi wa mtoto ni
mwiko kushirikishwa katika maziko.
Kwa mujibu wa Kidavashari watu wanne, wakiwemo wazazi wa marehemu
wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi ambapo watafikishwa
mahakamani mara tu baada ya upelelezi kukamilika.
Wengine wanaoshikiliwa na jeshi hilo ni Regina Kaboni na Msolwa Jacob (29), mkazi wa Kitongoji cha Mwikang’ombe.