Kampuni
ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), imefungua
kesi ya madai katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakimtaka
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe awalipe fidia ya Sh bilioni 500
kutokana na kutoa kashfa dhidi yao.
IPTL,
Kampuni ya Pan Africa Power Solutions Tanzania Limited (PAP) na
Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni hayo mawili, Harbinder Seth wamefungua
kesi dhidi ya Zitto, Mhariri wa gazeti la Raia Mwema, Kampuni ya Raia
Mwema na Kampuni ya Flint Graphics.
Washitakiwa
wengine wameshitakiwa kwasababu makala yenye maneno ya kashfa na
kuwachafua, iliyochapishwa Agosti 13 mwaka huu katika ukurasa wa 7 na 14
wa gazeti lao, ikiwa na kichwa cha habari cha “Fedha za IPTL ni Mali
ya Umma” na Kampuni ya Flint Graphics kwa kuchapisha gazeti hilo.
Aidha,
wanaiomba Mahakama iamuru makala hayo, yalikuwa ya upotoshaji na
kuwachafua kwa kudhamiria, pia wadaiwa waombe radhi kwa kuchapisha
habari ya kuomba msamaha kwenye kurasa za mbele katika matoleo mawili
mfululizo ya gazeti hilo.
Wadaiwa
hao waliiomba Mahakama, itoe zuio kwa wadaiwa, watumishi wao,
wafanyakazi, washirika, wawakilishi au watu wengine wanaofanya kazi
chini ya wadaiwa, kuchapisha au kuandika makala yoyote ya kuwachafua.
Wanadai makala hayo yalikuwa na maneno
“kwa mara nyingine Serikali kupitia viongozi wake akiwamo Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), wamedai kwamba dola milioni 250 za Kimarekani
zilizopaswa kuendelea kuwepo katika akaunti ya “Tegeta Escrow Account’
si mali ya Serikali na hivyo si mali ya umma…. Akaunti hiyo ilifunguliwa
na Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Tanesco
pamoja na IPTL”.
Ilidaiwa
kuwa kabla ya kusambaza habari hizo, wadaiwa walitakiwa kufanya juhudi
za kuthibitisha ukweli kutoka kwao au kwa maofisa husika wa Serikali,
ambao wangethibitisha ukweli kuwa fedha zilizowekwa kwenye akaunti ya
Escrow, zilikuwa ni dola milioni 122 za Kimarekani na siyo dola milioni
250, kama walivyodai.
Aidha,
wangejua fedha ziliwekwa katika makubaliano ya Escrow ;na siyo kama
fedha za umma, lakini ni kutokana na mgogoro wa malipo, yaliyotakiwa
kufanywa na Tanesco kwa IPTL.
Wadai hao walifungua kesi hiyo Septemba 4, mwaka huu kupitia kwa Wakili Melchisedeck Lutema na Kay Felician Mwesiga.