Uraia
pacha kwa Watanzania walioko nje ya nchi jana uliendelea kutawala
katika mijadala kwenye Bunge la Katiba huku wengi waliochangia
wakikubaliana wasio na uraia Katiba iruhusu wapewe chini ya utaratibu wa
uraia wa pacha.
Wachangiaji wengi walisema hakuna sababu ya kuwanyima uraia hao kwa kisingizio kuwa sio wazalendo.
Selemani
Ali alisema Watanzania walioenda nje ya nchi kusaka maisha umefika
wakati warejeshewe uraia wao kwani watapata fursa pia ya kufaidika na
matunda ya nchi yao.
Lakini
Luis Majaliwa alisema Watanzania hao hawana hadhi ya kupewa uraia kwa
sababu si wazalendo kwani walikimbia nchi kwa kuona maisha ni magumu na
kuwaacha wenzao wanahangaika kuikwamua nchi kwenye maendeleo.
Alisema, “iweje leo hii walioacha jahazi linazama waona mambo yanaenda vizuri waruhusiwe kuja kupewa tena uraia.” Alipendekeza Katiba isiwape hadhi ya kupewa uraia.
Mjumbe
Nyambali Nyangwine alisema Katiba isiweke masharti magumu kwa
Watanzania walioko nje ambao wanataka kupata uraia wa nchini.
Alisema umefika wakati wa Watanzania kubadilisha fikra na msimamo na mitizamo yao dhidi ya Watanzania walioko nje ya nchi.
Zakia
Meghji alisema walioko nje ya nchi ni Watanzania na wanafanya kazi na
sehemu ya fedha hizo wanazituma kwa jamii zao zilizoko nchini na
wanaweza kuja kuwekeza pia nchini.
Alisema
hakuna sababu ya kuwakatalia kuwapa uraia kwani walikana uraia wa hapa
nchini ili waweze kufaidika na elimu ya nje pamoja kupata ajira.
“Hapa tunatoa uraia kwa watu ambao siyo Watanzania, iweje tuwanyime watoto wetu uraia?” Alihoji Meghji.
Mussa Azzan Zungu alisema haoni sababu inayokera Watanzania hadi wawanyime Watanzania wenzao walioko nje kupatiwa uraia.
Hoja
hiyo pia iliungwa mkono na Jasson Rweikiza ambaye alisema umefika
wakati watu waachwe wawe na uraia wa nchi mbili ili kutoa fursa zaidi
kwa vijana wa kitanzania kwenda nje kusaka maisha.
Ave
Maria Semakafu alisema Watanzania hao walioko nje walienda huko kusaka
ajira kutokana na tatizo la ajira lililoko hapa nchini na akahoji
wakirudi wote hao ajira zitapatikana wapi?
Alishauri
mfumo wa kuwapatia uraia ukubaliwe kwani kwenda kwao nje ya nchi sio
kwamba walikosa uzalendo ila walienda kusaka maisha zaidi.
Zainabu Gama naye alikubaliana na hoja hiyo na akasema kwamba kuwanyima uraia Watanzania hao ni kuwaonea.