JESHI la Zimamoto na Uokoaji limedai kuwa askari wanafunzi 37
waliyofukuzwa mafunzoni katika chuo cha Magereza Kiwira, Tukuyu mkoani
Mbeya ni kutokana na kutokidhi vigezo mbalimbali tofauti na inavyodaiwa
kwamba wamekutwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU).
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa
Jeshi hilo, Inspekta Puyo Nzalayaimisi, alisema kama Jeshi wana taratibu
na vigezo ambavyo mtumishi anatakiwa kukidhi na hilo suala la kwamba
wana VVU halina ukweli wowote.
Akifafanua zaidi, Inspekta Nzalayaimisi, alisema hata kama ingetokea
mtu akakutwa katika hali hiyo, wasingeweza kumfukuza au kumtangaza mbele
ya watu kama ilivyodaiwa, kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume na maadili
ya utumishi wa umma.
Kwa mujibu wa Msemaji huyo, ili kuhakikisha watu wenye maambukizi
hawanyanyapaliwi, ndio maana katika bajeti hutenga fungu kwa ajili ya
kuhudumia watu wa aina hiyo.
Hata hivyo, alisema mojawapo ya vigezo ambavyo askari anaweza
kuondolewa kutokana na kutokidhi, ni pamoja na ugonjwa wa pumu au kifafa
kutokana na aina yao ya kazi wanayoifanya ya moto, hairuhusu watu wa
aina hiyo.
“Hebu niambie… kwa kazi yetu unaweza kumuajiri mtu ambaye anaanguka
kifafa aende akazime moto, na vitu kama hivi wananchi wanapaswa kujua
kwamba haviwezi kugundulika pale tunapowasaili, bali hujitokeza wakati
mwingine wakiwa kwenye mafunzo,” alisema.
Habari za kufukuzwa kwa wanafunzi hao, zililifikia Tanzania Daima Septemba 2 mwaka huu, kutoka katika chanzo cha kuaminika.
Chanzo hicho kilidai kwamba, taarifa za wenzao kutimuliwa
walitangaziwa majira ya saa 4:00 asubuhi baada ya kupata chai, ambazo
ziliwashtua sana na kuona huo ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Kiliongeza kuwa, cha kusikitisha zaidi ni kwamba wamebakiza wiki
mbili kumalizia masomo yao japokuwa kwa taratibu za mafunzo hayo
zinaeleza kuwa, huwa hawana muda maalum kwani hutolewa baada ya uongozi
kuona wameiva.
>>Tanzania daima