KIJANA Ally Selemeni (30), mkazi wa Mikindani, mkoani Mtwara
aliyeleta hofu kwa wananchi waliokuwepo katika maeneo ya hospitali ya
Rufaa ya Ligula kuwa ana dalili za ugonjwa wa Ebola, anaendelea vema na
imebainika hana ugonjwa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hospitali hiyo,
Selemani alisema kuwa alilazwa kutokana na
kusumbuliwa na kifua kwa miezi miwili sasa.
Selemani aliyasema hayo kutokana na uvumi uliojitokeza mkoani humo
kwamba ameathiriwa na ugonjwa wa ebola baada ya kutokwa na damu katika
mwili wake kupitia puani na mdomoni kitendo kilichofanya wauguzi
kumkimbia na kwenda kutafuta vifaa vya kujikinga na gonjwa huo.
“Watanzania wenzangu naomba wajue kuwa mimi sina ugonjwa wa ebola ila
ni maneno ya watu tu baada ya kuona natoka damu katika mwili wangu
wakajua nina huo ugonjwa,” alisema
Naye mdogo wa mgonjwa huyo, Sanjamin Abdallah (20) alisema kuwa kaka
yake anasumbuliwa na kifua na sio kwamba ameathiriwa na ugonjwa wa ebola
kama ilivyoelezwa na baadhi ya watu waliomuona.
Naye muuguzi aliyekuwepo zamu siku ya tukio, Mariam Mkanyama, alisema
kuwa walipoona mgonjwa huyo anatokwa na damu puani na mdomoni
walishitushwa na hali hiyo.
“Yaani tulipoona mgonjwa wa kifua anatoka damu puani na mdomoni
tulipata na mshtuko mkubwa na tulikimbia kwenda kuchukua vifaa vya
kujikinga zaidi kwa ajili ya kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo,”
alisema.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 27 mwaka huu saa 4 asubuhi
ikiwa ni siku ya tisa tangu mgonjwa huyu alazwe hospitalini hapo.