TANZANIA inatarajiwa kupata Sheria ya Uhuru wa kupata Habari ifikapo
Februari, mwakani. Rais Jakaya Kikwete alisema hayo jana alipokuwa mmoja
wa wazungumzaji katika mkutano unaohusu Uwazi na Ushirikiano kati ya
Serikali na Jamii.
Rais Kikwete alisema rasimu ya muswada wa Uhuru wa kupata Habari uko
katika hatua ya mwisho ambapo wadau mbalimbali wanashauriana na kutoa
maoni tayari kupelekwa bungeni.
Oktoba mwaka jana, katika mkutano wa Open Government Partnership
(OGP) jijini London, Rais Kikwete alitangaza nia na ujasiri ulioko
serikalini kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na sheria ya uhuru wa
habari.
Alisema uhuru wa habari ni muhimu kwa wananchi kwa sababu: "Ni haki
yao ya msingi na kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi yanayofaa kuhusu
maisha yao," na kuongeza: "Ni muhimu wananchi kujua serikali yao
inafanya nini kwa niaba yao".
Akizungumza katika mkutano huo jana, Rais Barack Obama wa Marekani
alisema OGP ni ubia kati ya Serikali na wananchi wake. Viongozi wengine
waliochangia katika mkutano huo ni pamoja na wa Indonesia, Afrika Kusini
na Ufaransa.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amekutana na Waziri Mkuu wa zamani wa
Uingereza, Gordon Brown ambaye pia ni Mjumbe Maalumu wa UN kuhusu elimu
ambaye amemshukuru na kumsifu Rais Kikwete kwa kusimamia elimu nchini.
Wabia hao ni pamoja na Shirika la Global Education, Shirika la Watoto
Duniani (UNICEF), Shirika la Misaada la Marekani (USAID), wawakilishi
wa Serikali ya Uingereza na Benki ya Dunia.
Wengine ni kutoka Global Business Coalition na Dubai CARES ambao kwa
pamoja wanataka kuinua kiwango cha Elimu ya Msingi na Sekondari kwa
kusaidia na kuchangia ili kuboresha zaidi na kuinua kiwango cha elimu
nchini.
0 Comments