ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Method Kilaini
amesema kukataa uraia pacha ni sawa na kukubali kupoteza watoto na nchi
kubaki kama kisiwa wakati nchi nyingine zinafanya hivyo, jambo ambalo
Watanzania wengi watakimbilia uraia wa nchi nyingine.
Alisema watafanya hivyo kwa lengo la kupata kazi, ikiwa ni pamoja na
kupoteza wanamichezo ambao wanaenda nje ya nchi kwa ajili ya masilahi.
“Mimi naona hili lingeruhusiwa bali kuwa masharti ya kutogombea
nafasi yoyote ya uongozi ni vema tukaangalia nchi kama Marekani
wanavyonufaika na suala hilo,” alisema.
Akizungumzia suala la Zanzibar kuruhusiwa kujiunga na mashirika ya
kimataifa, alisema hakubaliani nalo, kwani suala hilo linafanya kusiwe
na maana ya Muungano.
Alisema haiwezekani kusema Zanzibar, si nchi wakati inakuwa na sera
mbili ya kujiamulia mambo yake na yale ya muungano, jambo ambalo ni
hatari kwa ajili ya usalama wa nchi. Haki za binadamu Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen-Kijo
Bisimba alisema hajaridhishwa na mchakato mzima wa Katiba hadi sasa.
Pia, alisema Rasimu hiyo mpya haijagusa eneo la haki za binadamu.
Alisema katika Rasimu zote za awali ya kwanza na ya pili, zilibainisha
kipengele kinachoelezea mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu
kuibana dola ili iweze kutekeleza haki za binadamu.
“Lakini nashangaa katika rasimu hii mpya kipengele kilichopo Ibara ya
53 (3) inaelezea juu juu tu suala la haki za binadamu bila kuitaka
mikataba hii kama sisi wadau na wananchi tulivyochangia, hii haina maana
kabisa,” alisema Bisimba.
Mawaziri kuwa Wabunge Katika eneo hili, Askofu Kilaini alisema rasimu
hiyo ya BMK ina vipengele vingi ambayo anaamini kuwa wananchi
watavikataa ikiwa ni pamoja na yeye kama mawaziri kuwa wabunge na
kutoruhusu wananchi kuwaondoa wabunge ambao hawawaridhishi.
Alisema kipengele hicho ingefaa mawaziri kuwa na kazi moja tu ya
utendaji Serikalini na kueleweka hivyo na siyo kujiingiza katika siasa
pia.
Dk Bisimba alisema pia katika rasimu hiyo aliyoiita mpya, Bunge hilo
Maalum la Katiba limeondoa maeneo yote yanayowagusa kwa namna moja ama
nyingine huku akitolea mfano eneo la uwajibikaji.
Alisema katika eneo hilo katika rasimu za kwanza zilibainisha kuwa
wabunge kwa kuwa wabunge wengi hawafanyi vizuri katika kipindi chao cha
miaka mitano cha kuwatumia wananchi kutokana na kutoguswa kisheria,
Katiba mpya itamke wazi kuwa mbunge atakayeshindwa kuwatumikia wananchi
aondolewe achaguliwe mwingine.
Alisema katika rasimu hiyo mpya kipengele hicho kimeondolewa na
kwamba mbunge bado anaendelea kuwatumia wananchi kwa kipindi chote bila
kufanywa lolote hata kama hawajibiki.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Shule ya Uandishi wa Habari na
Mawasiliano ya Umma, Ayoub Rioba, alisema Bunge hilo la Katiba ni kama
vile limetunga rasimu mpya kwa kuwa limezifanyia mapinduzi rasimu zote
zilizopita.
“Mchakato wote una tatizo, ulianza na kuundwa kwa tume ya Rais
kukusanya maoni, maoni hayo yakatengenezewa rasimu, ambayo ikapelekwa
bungeni ambako Bunge lingeirudisha kwa wananchi, lakini ikiwa bungeni
imefanyiwa mapinduzi kwa kweli sina la zaidi,” alisema Rioba.
Mambo ya Muungano Kuhusu mambo ya Muungano, Mkurugenzi wa Utetezi
maboresho na Sheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),
Harold Sungusia alisema kuongezeka kwa masuala hayo kunatokana na
kubomoa uliokuwa muundo wa serikali tatu na kuwa mbili.
Anasema misingi ya mambo ya katiba yanatokana na muundo, uliokuwepo
tangu mwaka 1964 na kwamba jambo la muhimu wangeyavunja hayo kwanza
kabla ya kuongeza hayo yaliyoongezeka.
Alisema suala zima la Muungano, lingerudishwa kwa wananchi na kupigiwa kura kwanza kabla ya kuhitimishwa katika rasimu hiyo.
Mambo hayo ya Muungano yaliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba ni
pamoja na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na usalama,
usalama na usafiri wa anga, urais na uhamiaji, jeshi la polisi, sarafu
na benki kuu, kodi ya mapato inayolipwa a watu binafsi na mashirika na
ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zilizotengenezwa nchini na
kusimamiwa na idara ya forodha.
Mambo mengine ni mambo ya nje, usajili wa vyama vya siasa, mahakama
ya juu na mahakama ya rufani, elimu ya juu, baraza la taifa la mitihani
na mambo yote yanayohusika na baraza hilo, utabiri wa hali ya hewa na
utumishi katika serikali ya jamhuri ya Muungano.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya hali ya Hewa
nchini (TMA) Dk Agnes Kijazi alipongeza kuongezeka kwa mambo ya
Muungano, kwani kutatoa mwanya mpana wa kufanya kazi za hali ya hewa.
Alisema suala la hali ya hewa halina mipaka, ambapo kuwa mojawapo katika
Muungano litasaidia katika uwekaji wa vifaa na kutoa taarifa za hali ya
hewa kwa wote.
Aidha, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania
(TGNP), Ussu Mallya alipongeza rasimu hiyo kuzingatia kwa kwa kiwango
kikubwa suala la usawa wa jinsia.
Alisema yapo mengi yaliyozingatiwa yanayohusu usawa wa jinsia
likiwemo la uwakilishi katika uongozi, haki mbalimbali katika kumiliki
na kutumia ardhi, afya ya uzazi salama, umri wa mtoto wa kike
kufafanuliwa, kutambua lugha mbadala za alama kwa ajili ya watu wenye
ulemavu pia na haki za makundi mbalimbali.
0 Comments