Mahakama ya Wilaya ya Ilala imemhukumu kifungo cha miaka sita jela,
Melkiad Kabunduguru(28) baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia fedha
kwa njia ya udanganyifu na kukutwa na noti bandia.
Kabunduguru ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma(Udom)
atatumikia kifungo hicho baada ya Mahakama kuridhika na ushahidi
uliotolewa dhidi yake.
Katika shtaka la kwanza la Kabunduguru atatumikia kifungo cha miaka
minne baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia fedha kwa njia ya
udanganyifu huku shtaka la pili la kukutwa na noti 50 za bandia za
Sh5000 mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka miwili.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Juma Hassani alisema mshtakiwa
atatumikia vifungo hivyo kwa pamoja baada ya Mahakama kuridhishwa na
ushahidi uliotolewa mahakamani.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Juma Hassani alidai kuwa mshtakiwa
huyo atatumikia kifungo hicho ili iwe fundisho kwa vijana wengine wenye
tabia za wizi.
Kabla ya kutoa hukumu hiyo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mwendesha
mashtaka, Felista Mosha uliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa
mshtakiwa ili iwe fundisho kwa vijana wengine wenye tabia za
udanganyifu.

“Mheshimiwa hakimu naiomba mahakama hii tukufu kutoa adhabu kali dhidi ya mtuhumiwa huyu kutokana na kushamiri kwa vitendo vya udanganyifu na kujihusisha na matumizi ya noti bandia wakati akijua kuwa ni kosa la kisheria,” alidai Mosha .
Baada ya Hakimu Hassani kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, alimuhukumu Mwiganyi kifungo cha miaka sita jela.
Awali, Wakili wa Serikali, Felista Mosha alidai mahakamani hapo kuwa
mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 29, mwaka huu katika Barabara la
Ally Hassan Mwinyi katika mashine ya kutolea fedha (ATM) ya NMB iliyopo Chuo cha Biashara (CBE) na kujipatia Sh100,000 kutoka kwa Expedith Mtisi kwa madai kuwa angemrejeshea lakini hakufanya hivyo.
Katika shtaka la pili, mshtakiwa alikutwa na noti bandia 50 za Sh5000.
0 Comments