Advertisement

Responsive Advertisement

SIMBA SC NI BALAA SANA...KIONGERA MBILI, MESSI MOJA, GOR MAHIA YALALA 3-0

Wauaji; Paul Kiongera kulia akipongezwa na Ramadhani Singano 'Messi' baada ya kufunga bao la tatu

Mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi akiichezea kwa mara ya kwanza timu yake zamani, Simba SC alijikuta katika wakati mgumu kutokana na kuzomewa kila alipogusa mpira na mashabiki wa Yanga SC aliowakimbia kurejea Msimbazi.
SIMBA SC imeonyesha ubora wake wa msimu huu, baada ya kuwafumua mabingwa wa Kenya, Gor Mahia mabao 3-0 katika mchezo wa kirafiki jioni hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mabao ya Simba SC yote yamepatikana kipindi cha pili, wafungaji Paul Kiongera aliyeiadhibu mara mbili timu yake ya zamani na Ramadhani SIngano ‘Messi’ moja. ITAENDELEA.
Hata hivyo, mwanzoni ilimpa tabu Okwi na kushindwa kucheza vizuri, ili baadaye akatulia na kujikuta anakuwa chachu ya ushindi wa Simba SC.
Gor Mahia walianza vizuri wakitawala mchezo hususan eneo la kiungo, lakini safu imara ya ulinzi ya Simba SC chini ya Nahodha Joseph Owino ilikuwa kikwazo kwao kupata mabao na sifa zaidi zimuendee kipa Ivo Mapunda aliyeokoa michomo mingi ya hatari.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Patrick Phiri dakika ya 34 kumtoa kiungo mkabaji William Lucian ‘Gallas’ na kumuingiza winga Uhuru Suleiman aliyekwenda kucheza pembeni kwa Awadh Juma aliyeingia ndani, yaliibadilisha Simba SC kwa ujumla.
Okwi akaingia ndani na Uhuru akawa anashambulia pembeni kushoto, Singano Messi kulia-na hapo Simba SC ikawa moto kwa Gor.
Phiri alianza na mabadiliko kipindi cha pili akimpumzisha mshambuliaji Elias Maguri na nafasi yake kuchukua Mkenya, Paul Kiongera, aliyekuwa shujaa wa mchezo.  
Emanuel Okwi akimtoka Kennedy Opiyo wa Gor Mahia


Kiongera alifunga bao la kwanza dakika ya 52 akiunganisha krosi ya Okwi aliyemlamba chenga na kumtoroka vizuri beki wa Gor pembeni kushoto.
Messi akafunga la pili dakika ya 67 akiuwahi mpira uliotemwa na kipa Frederic Onyango kufuatia shuti la Okwi aliyemalizia krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’ kabla ya Kiongera kumalizia vizuri krosi ya Uhuru dakika ya 78 kuipatia Simba SC bao la tatu.  
Kwa Kiongera huu unakuwa mchezo wa pili tangu ajiunge na Simba SC baada ya awali kucheza katika Simba Day, Wekundu wa Msimbazi wakifungwa 3-0 na Zesco United ya Zambia.
Kwa kocha Phiri, huu unakuwa mchezo wa nne tangu arejee Simba SC mwezi uliopita na ameshinda mechi zote, awali 2-1 na Kilimani FC, 2-0 na Mafunzo na 5-0 na KMKM, zote za Zanzibar.
Kikosi cha Simba SC leo kilikuwa; Ivo Mapunda, Miraj Adam/Nassor Masoud ‘Chollo’ dk70, Abdi Banda/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk55, Hassan Isihaka, Joseph Owino, William Lucian ‘Gallas’/Uhuru Suleiman dk34, Awadh Juma, Shaaban Kisiga ‘Malone’/Abdallah Seseme dk86, Elias Maguri/Paul Kiongera dk46, Emmanuel Okwi/Ibrahim Ajibu dk 77 na Ramadhani Singano ‘Messi’/Twaha Shekuwe ‘Messi’ dk77.

Gor Mahia; Frederic Onyango, Mussa Mohamed, Kennedy Opiyo, Haruna Shakana, David Owino, Daniel Onyango/Charles Bruno dk74, Simon Mburu/George Odhiambo dk65, Erick Ochieng, Patrick Onyango/Joseph Kariuki dk55, Dani Sserunkuma na Timoth Otieno/ian Niva dk88.