WAJAWAZITO katika Kijiji cha Chamgoi, Kata ya Mkamba, wilayani
Mkuranga, Pwani, wamekuwa wakijifungua njiani kwenye matenga kutokana na
kukosa kituo cha afya.
Hayo yalibainika juzi kijijini hapo, baada ya Kamati ya siasa ya Chama
cha Mapinduzi (CCM), kufanya ziara katika Kata hiyo kwa lengo la
kuangalia utekelezaji wa ilani ya chama hicho.
Akizungumza kijijini hapo, Amina Abdalla,
alisema hali hiyo inasababisha watoto wanaozaliwa kupoteza maisha
kutokana na kukosa huduma ya kwanza pindi wanapozaliwa.
“Tunapotaka kujifungua tunaenda umbali wa saa tatu kufuata huduma
hiyo, katika vituo vya jirani, usafiri hakuna hali inayotulazimu
tupakiwe kwenye baiskeli au pikipiki ambapo tunawekwa kwenye
tenga,”alisema.
Diwani wa kata hiyo, Hassan Dunda, alisema mpaka sasa wananchi
wamejichangisha sh milioni 17 kwa ajili ya ujenzi wa zahati katika
kijiji hicho na kwamba kwa sasa imefikia hatua ya kuweka milango na
madirisha.
“Chamgoi hatujaridhishwa na serikali kutowaunga mkono wananchi, natoa
wito kwa wanakijiji, msikimbilie kuchagua viongozi ambao wanaomba
uongozi bila kujipima uwezo wao wa kuwatumikia alisema Dunda ambaye pia ni Katibu Mwenezi wilayani humo.