MDAHALO wa kujadili Katiba inayopendekezwa ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, jana ulivunjika baada ya kutokea vurugu ambako Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alipigwa vibao shingoni na watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa CCM.
Hali hiyo ilijitokeza kwenye Hoteli ya Blue Pearl iliyopo Ubungo
Dar es Salaam, baada ya kuvunjika mdahalo huo uliokuwa umehudhuriwa na
mamia ya watu, wengi wao wakiwa vijana.
Baada ya vurugu hizo, waandaji waliamua kuwatoa nje ya ukumbi
wasemaji wa mdahalo huo akiwamo Warioba, Mwenyekiti wa Taasisi ya
Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, Profesa Palamagamba Kabudi na Profesa
Mwesiga Baregu.
Wengine waliokuwa wazungumze kwenye mdahalo huo ni Humphrey
Polepole na Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, Awadhi Said, ambao
wote walikuwa wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Warioba, aliyewahi kushika wadhifa wa Waziri Mkuu na Makamu wa
Rais, alipigwa vibao viwili shingoni alipofika kwenye mlango kuu wa
kutoka ukumbini ambako kulikuwa na msongamano mkubwa wa watu. Wakati
huo, Warioba na viongozi wenzake walikuwa wakitolewa nje ya ukumbi huo.
Hatua hiyo ilifanya mlinzi wake na baadhi ya watu waliokuwa wakimtoa
kiongozi huyo waongeze mwendo na kumkimbiza kiongozi huyo wa taifa
kwenye chumba maalumu cha wageni wa heshima (VIP lounge), kilichoko
ndani ya hoteli hiyo.
Wakati Warioba akipigwa vibao, miongoni mwa watu waliokuwa karibu nyuna yake ni Katibu wa Uhamasishaji wa UVCCM, Paul Makonda.
Kwa sababu hiyo, baadhi ya vijana walichangia kumpiga kada huyo wa
UVCCM aliyekuwa amevalia shati jeupe, huku wakimzuia kuingia kwenye
chumba cha VIP ambako Jaji Warioba alikuwa amepelekwa.
Kufanikiwa kwa vijana hao kumzuia Makonda kuingia kwenye chumba
hicho, kulitoa fursa ya kuendelea kupigwa hadi alipoponyoka na
kukimbilia katika ofisi moja katika jengo hilo na kujifungia.
Baada ya kujificha katika chumba hicho, vijana hao waliitana na kuhamasishana ili wavunje mlango huo na kumtoa Makonda.
Hata hivyo baada kufanikiwa kuvunja mlango huo, vijana hao
hawakumuona Makonda hadi walinzi wa hoteli hiyo na askari kanzu
walipofika hapo na kuwafukuza.
Vurugu zilivyoanza
Vurugu katika mdahalo huo zilianza muda mfupi kabla ya Jaji Warioba aliyekuwa msemaji wa kwanza, kumaliza hotuba yake.
Baada ya kumaliza kuichambua Katiba inayopendekezwa, Jaji Warioba
alisema katika kuitetae katiba hiyo, baadhi ya watu wamekuwa wakimtumia
Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere kuunga mkono hoja zao.
“Tunatumia jina la Mwalimu ili kuunga mkono hoja zetu wakati mwingine ninajiuliza hivi tunatumia Mwalimu yuleyule ama…
“Mwalimu amekufa akisema hajaona hata sehemu ya kutia koma katika
Azimio la Arusha, kuna watu waliwahi kumletea Mwalimu barua wakimwambia
afungue akaunti nje ya nchi ndiyo fedha zake zitakuwa salama… Mwalimu
siyo tu alikataa lakini alitangaza kila kitu hadharani.
“Leo Mwalimu angekuwapo angekubali watu wafungue akaunti nje ya
nchi, angekubali watu wapewe zawadi wakae nazo… nikasema huyo wao siyo
Mwalimu, Mwalimu alikuwa ni mtu mwenye uwezo wa kufanya uamuzi mgumu
hata unaomhusu yeye,” alisema Warioba.
Vijana na mabango
Baada ya maneno hayo, baadhi ya vijana takriban 20, walisimama na
kunyanyua juu mabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali wa kumtukana Jaji
Warioba na mengine yakisifu Katiba inayopendekezwa.
Kitendo hicho kilifanya baadhi ya watu kujaribu kuwakalisha chini huku wengine wakichana mabango hayo hali iliyozusha vurugu.
Wakati wote huo Jaji Warioba alikuwa amesimama akijaribu kuwasihi
watu hao kukaa chini, lakini hali hiyo ilionekana kutozaa matunda.
Baada ya muda vijana hao walijitenga pembeni karibu na jukwaa kuu
huku wakiwa na mabango yao, wakiimba nyimbo mbalimbali za CCM.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya watu watoke ukumbini huku wengine wakiwa wanarudi kuketi kwenye viti vyao.
Wakati vurugu hizo zikiendelea, Profesa Kabudi na Butiku kwa nyakati
tofauti, walionekana wakimtaka Makonda kuwatuliza vijana hao wa CCM
ambao alidaiwa yeye yeye ndiye aliwaingiza katika ukumbi huo.
Wakati viongozi wakimtaka Makonda kufanya hayo, vijana wengine
walionekana kumvuta Makonda wakitaka kumpiga hali iliyomlazima kumtumia
kama kinga, Amon Mpanju, ambaye alikuwa Mjumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba akiwakilisha kundi la walemavu.
Hali iliendelea hivyo hadi baadhi ya vijana waliokuwa wamekaa
walipohamasishana na kuwapiga wale waliokuwa na mabango, kwa kutumia
viti hali iliyofanya wakimbie na kutoka nje ya ukumbi huo.
Baada ya vijana hao kutoka nje, hali iliwageukia Makonda na Mpanju
ambao baada ya kuona hali imekuwa tete, walikimbilia kwenye jukwaa kuu
na kukaa karibu na Jaji Warioba.
Huku hali ikiwa bado ya taharuki, viongozi hao (Warioba na wenzake)
waliamua kutoka nje ya ukumbi na ndipo zahama ya kupigwa vibao kwa Jaji
Warioba ilipojitokeza.

0 Comments