Mfano wa usafiri waliotumia kufika eneo la tukio japokuwa yeye anadai alikuja na usafiri wa Chungu |
Katika hali isiyokuwa ya kawaida binti anayekadiriwa kuwa na
umri wa miaka 23- 25 anayedaiwa kuwa ni mchawi amekutwa kwenye nyumba ya mtu
katika mtaa wa Bushushu kata ya Lubaga katika manispaa ya Shinyanga akiwa
amevaa kishirikina na mwili wake ukiwa umepakwa dawa nyeusi akidai alikuwa
anaongoza wenzake zaidi ya 10 kutoka kanda ya ziwa kuwanga katika nyumba hiyo.
Tukio
hilo lililovuta hisia za mamia ya wakazi wa Shinyanga
limetokea jana asubuhi nyumbani kwa Robinson Massawe mfanyabiashara wa
duka la dawa za binadamu mjini Shinyanga ambapo binti huyo alikutwa
amelala mbele ya mlango wa nyumba hiyo akiwa hajitambui na baada ya
kusemeshwa
ndipo akasimulia yaliyomkuta kwamba alifika mahali hapo na wenzake zaidi
ya 10
kufanya sherehe baada ya kufanikisha uchawi wao.
Mashuhuda wa tukio walisema baada ya kumhoji binti huyo
alisema alifika kwenye familia hiyo,akiwa kiongozi wa kundi la wachawi zaidi ya
10 kutoka Ushirombo,Misungwi na Shinyanga saa 9 usiku kwa ajili ya kufanya
sherehe baada ya kufanikiwa kusambaratisha kichawi ndoa ya Massawe na Mary
Joseph.
“Tumemkuta hapa anasema leo ni mara ya tatu wanakuja kufanya
uchawi wao,lengo lao ni kutaka ndugu yao aolewe na Massawe,walikuja siku ya
kwanza wakakuta mke wa Massawe akisali,wakashindwa,wakarudi mara ya pili kwa
ajili ya kusambaratisha ndoa,wakafanikiwa leo walikuja kufanya sherehe kwa kazi
hiyo lakini wenzake wamemkimbia”,alieleza Stella Joseph mdogo wa mke
aliyeachika.
“Anadai
kuwa Robinson alitoa ahadi ya kumuoa mwanamke ambaye ni ndugu yao
badala yake akaoa mwanamke mwingine,aliyeahidiwa kuolewa katoa taarifa
kwa mama mdogo wake ambaye ni mchawi,naye kalifikisha kwa wakuu
wake,wakaamua
kuingia kazini kutaka ndoa kishirikina”,aliongeza Hamis Juma.
Akizungumza na Malunde1 blog iliyofika eneo la tukio haraka sana tena kawaida yake,binti huyo anayedaiwa kuwa
mchawi aliyejitambulisha kwa jina la Coletha akizugumza kwa lugha ya Kisukuma kutoka Ushirombo mkoani Geita,
alisema alikuwa anaongoza kundi la wachawi kutoka Mwanza,Geita na Shinyanga
lakini wakazidiwa nguvu wenzake wakamkimbia.
“Mimi ni mdogo sana kwa wachawi wenzangu,siyo mzoefu sana,walinitanguliza
mbele ,nilipodondoka na chungu change wenzangu wakanikimbia,nimebaki peke
yangu,kila mmoja amekuja na usafiri wake,mimi nimekuja na chungu,wengine
wamekuja na ungo”,alieleza Binti huyo.
"Baba mwenye nyumba hii alitoa ahadi ya kuoa mtoto wa mshirika mwenzetu(mama mdogo wa binti),na mama mdogo huyo ndiyo akaleta malalamiko kwa wachawi kuwa tumshughulikie huyu baba anayechezea watoto wa watu",aliongeza.
Naye mwenyekiti wa mtaa wa Bushushu Ruben Masanja aliyefika
eneo la tukio alisema ni kweli ndoa ya Robinson na Mary imevunjika tangu mwezi
Septemba mwaka 2014 na sasa baba wa familia hiyo anaishi na ndugu zake.
Masanja aliongeza kuwa huenda binti huyo ni mchawi kutokana
na maelezo yake na vitendo vilivyotokea katika familia hiyo huku akiwasihi
wakazi wa eneo hilo kutomwadhibu binti huyo kisha kumwingiza ndani ya nyumba
kusubiri polisi kwa ajili ya usalama wake.
“Anasema walikuja kufanya sherehe baada ya kumaliza kazi ya
kuvuruga ndoa,na kweli wanandoa wametengana tangu tarehe 17 Septemba 2014,sasa
wachawi hao wanataka ndugu yao aliyeahidiwa kuolewa na Robinson aolewe,binti
anayetaka kuolewa alitoa taarifa kwa mama mdogo wake ambaye ni mchawi,huyo mama
akatoa taarifa kwa wachawi wenzake ili washughulikie suala hilo”,Masanja aliiambia Malunde1 blog
Hata hivyo katika hali ya kushangaza watu mwanzo kufika
katika eneo la tukio walitoweka na vipande vya chungu alichodondoka nacho binti
huyo.
Kufuatia tukio hilo askari wa jeshi la polisi mkoa wa
Shinyanga walifika eneo la tukio na kumchukua binti huyo kwenye gari la polisi.
Tukio hili la binti kukutwa akiwanga nyumbani kwa mtu limetokea
siku chache tu baada ya bibi asiyejulikana makazi yake mwenye umri wa miaka 80
kukutwa uchi nje ya nyumba ya mtu katika kata ya Ndembezi manispaa ya
Shinyanga.
0 Comments