KUNA kasumba
ya kizamani kuwa wanaume ndiyo waliokuwa wanawapiga wake zao lakini
inavyoonekana sasa kibao kimegeuka baada ya mwanamke aliyejitambulisha
kwa jina la Irene Edwin kudaiwa kumzaba mumewe, Amani Joseph, wote
wakazi wa maeneo ya Misungwi mkoani hapa kisa kikielezwa kuwa ni wivu wa
kimapenzi.
Irene Edwin akimshushia kichapo mumewe.
Tukio hilo lililoshuhudiwa mchana kweupe lilijiri hivi karibuni maeneo
hayo ambapo Irene alimfuma mumewe akiwa baa na mchepuko wakiponda
raha.Kwa mujibu wa shuhuda wetu ambaye ni mtu wa karibu wa wanandoa hao,
mwanaume huyo alidaiwa kuwa na kawaida ya kutoka na mchepuko wake ambao
jina lake halikupatikana mara moja na kwenda kujiachia sehemu
mbalimbali za starehe hivyo kumfanya mkewe aweke mtego wa kuwanasa
wawili hao.
“Mwanzoni Irene alikuwa akisikia tu maneno kwa watu lakini ili apate
uhakika alianza kumfuatilia mumewe na kumwekea mtego ndipo akamnasa
mchana kweupe,” alidai shuhuda huyo.Shuhuda huyo aliendelea kumwaga
‘ubuyu’ kuwa baada ya mke kufika eneo la tukio aliwakuta wawili hao
wakiendelea kula raha ndipo alipoamua kuanzisha timbwili zito.
“Yaani Irene alipowanasa alimkamata kwanza mchepuko wa mumewe ili
autwange lakini ulimponyoka na kukimbia ndipo alipoamua kumshushia
kipondo kizito mume wake.“Baada ya timbwili kuwa zito walitoka nje ya
baa na kuendelea kuzichapa huku mwanaume akizidiwa nguvu na kujikuta
akizabuliwa na mkewe,” alisema shuhuda huyo.
Ilisemekana kwamba baada ya mume huyo kuzidiwa na kipigo hicho alisikika
akisema: “Niache tukayamalize nyumbani.” Hata hivyo, pamoja na utetezi,
mke hakutaka kumwelewa kwani aliendelea kumpa kibano hadi jamaa
alipotoka nduki.Huku akiwa na hasira, Irene alisema kuwa aliamua kufanya
hivyo kwani alikuwa amechoshwa na vitendo hivyo.
0 Comments