MTOTO Jacqueline
Lepenza, aliyenusurika katika ajali mbaya ya basi lililogongana na lori
huko Mafinga mkoani Iringa wiki mbili zilizopita, ameripotiwa kuwa na
maajabu baada ya baba yake mzazi kujitokeza na kusimulia, Uwazi
linakutaarifu.
Jacqueline Lepenza, akiwa na baba'ke.
Willy Lupenza, baba mzazi wa mtoto huyo mwenye umri wa miaka mitatu na
nusu, alisema marehemu mke wake, Anjela Osward (35) (pichani) alikuwa
amekwenda nyumbani kwao Ilembula mkoani Njombe kwa ajili ya ubatizo wa
binti yao huyo.
Alisema katika hali ya kushangaza, siku ya ubatizo huo, Jacqueline
alibatizwa peke yake pasipo watoto wenzake kupewa baraka hizo kwa sababu
ambazo hazikueleweka.“Ndugu mwandishi, hili ni tukio ambalo sitalisahau
katika maisha yangu, kwa sababu haiwezekani mtoto abatizwe peke yake
halafu kwenye ajali, idadi kubwa ya watu wapoteze maisha lakini yeye
anusurike.”
Alisema baada ya ajali, mtoto wake huyo alikutwa na watu waliojitokeza
kuwasaidia majeruhi akiwa amelala juu ya bati la kuzuia matope kwenye
tairi ya lori lililokuwa limebeba kontena huku akilia na matairi
yakiendelea kuzunguka.
Alisema haelewi mtoto huyo alitokaje ndani ya basi hadi kwenye bati hilo
la lori, kwani licha ya kukutwa mzima, lakini eneo hilo pia lilikuwa
hatarishi kwa mwanaye ambaye alimpoteza mama yake aliyekuwa mmoja kati
ya watu zaidi ya 50 waliofariki dunia.
...Akiwa na bibi yake.
Willy alisema Machi 11, mwaka huu alipata taarifa kwa njia ya simu
kutoka kwa shemeji yake ambaye yuko mkoani Iringa kwa shughuli zake za
kibiashara juu ya tukio hilo, baada ya yeye naye kuarifiwa na Jeshi la
Polisi Iringa baada ya kuokotwa kwa simu ya mkewe.
Alisema baada ya kupigiwa na polisi waliofika katika eneo la tukio
mapema, shemeji yake huyo alimpigia na kumjulisha juu ya mkewe kupata
matatizo Mafinga.“Nilianza safari mara moja kuelekea huko, lakini
nilipofika Morogoro nilipata taarifa za uhakika zilizoniaminisha kuwa
mke wangu alikuwa amefariki dunia,” alisema.
Aliongeza kuwa aliendelea kufanya mawasiliano na ndugu kujua alipo
mtoto, hadi alipoambiwa kuwa kulikuwa na mtoto mmoja aliyekuwa wodini
(Hospitali ya Wilaya Mafinga), hivyo akaambiwa kama anaweza kuwatumia
picha yake kwa njia ya mtandao ili waweze kumfananisha.
“Niliwatumia picha kwa Mtandao wa WhatsApp, kumbe siku ya ajali mwanangu
alikuwa amevaa gauni ambalo aliwahi kulivaa siku za nyuma, na ndiyo
picha niliyowatumia, walimtambua kirahisi na alipofanyiwa uchunguzi wa
kidaktari ikagundulika kuwa hakuwa na matatizo yoyote kiafya,” alisema
baba huyo.
Mamam wa Jacqueline, Anjela Osward enzi za uhai wake.
Kufuatia kufika Mafinga na kuutambua mwili wa mke wake, aliomba mwili
huo kutopelekwa sehemu yoyote ili urudishwe nyumbani kwao Ilembula kwa
mazishi yaliyofanyika katika Kijiji cha Mwambaga.Kuhusu hali ya mtoto
kwa sasa, Willy alisema anaendelea vizuri na anamshukuru Mungu pamoja na
madaktari na polisi walioshiriki katika tukio hilo ambalo mwanaye huyo
alipona kimaajabu.
Ajali hiyo ilihusisha lori aina ya Scania namba T 689 APJ mali ya Cipex
Company lililokuwa likiendeshwa na Maka Sebastian (26) na basi aina ya
Scania namba T 438 CED mali ya Majinja lililokuwa likiendeshwa na Baraka
Gabriel (38).
0 Comments