HUU ni ukatili uliopitiliza! Mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina
la Neema Mwita, anateseka katika Hospitali ya Mkoa wa Mara kufuatia
jereha kubwa alilopata baada ya mumewe aliyemtaja kwa jina la Juma Mwita
kummwagia uji wa moto kisa kikiwa ni kuchuma mahindi shambani bila
ridhaa ya mumewe huyo.
Akizungumza na Uwazi huku akimwaga machozi kila wakati, mwanamke huyo
alisema siku ya tukio, yeye na mumewe walikuwa kazini na mwanaume huyo
ambaye alipata tenda kubwa ya kufyatua matofali.
MSIKIE MWENYEWE
“Nilikuwa
nakusanya majani. Baada ya kukusanya kwa muda mrefu ambapo niliagizwa
na mume wangu, niliamua kwenda shambani kuchuma mahindi kisha nikarudi
nyumbani kupika chakula cha mchana ili akitoka kazini ale.
“Nikiwa jikoni nasubiri uji uchemke ili nisonge ugali, mume wangu
alirudi ghafla na kuanza kunigombeza eti kwa nini nilichuma mahindi
shambani na nilirudi nyumbani bila ridhaa yake?” alisema na kuanza
kulia.
MUME ACHUKUA UJI WA UGALI
Mwanamke
huyo aliendelea kusema: “Alinihoji ni kazi gani kubwa niliyoifanya kule
kwenye matofali mpaka nikaamua kurudi nyumbani. Kabla sijajibu
aliifuata sufuria yenye uji unaochemka jikoni na kunimwagia ambapo
ulitua kifuani kwangu na kuniunguza vibaya, kama unavyoona. Sijajua mume
wangu alikusudia nini kunifanya hivi!”
JIRANI AMWOKOA
Mwanamke
huyo aliendelea kusema kuwa, baada ya kumwagiwa uji huo na kuungua,
alianguka chini na kulia kwa maumivu, ndipo jirani yake mmoja alimwona
akihangaika na kumchukua hadi ndani.
AKAA NYUMBANI SIKU SABA
“Ndani
nilikaa kwa wiki nzima, maumivu yalikuwa makali sana. Ndipo wazazi
wangu walipopata taarifa wakaja kunichukua. Hata hivyo, wazazi wangu nao
hawakunipeleka hospitali, waliniweka nyumbani na kuniletea mganga wa
kienyeji.”
MUME AKIMBILIA KUSIKOJULIKANA
Neema
alisema mumewe aliyeoana naye kwa upendo na kiapo cha kuishi katika
shida na raha mpaka kufa, alikimbia baada ya tukio hilo na hajawahi
kuonekana mpaka sasa ambapo polisi wanaendelea kumsaka usiku na mchana.
TAARIFA ZINAFIKA SERIKALINI
Mwanamke
huyo ambaye kutokana na kuungua huko mishipa yake ya sehemu ya kidevuni
imeshikana na ya shingo, alisema baada ya wiki moja, taarifa zilimfikia
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamisanga, Boke Chacha ambaye alimchukua
mikononi mwa wazazi hao na kumpeleka hospitali kwa matibabu.
LICHA YA KUUNGUA, AMETELEKEZWA
Neema,
anasikitisha sana kwani licha ya kupitia kipindi hicho kigumu, anadai
ametelekezwa na wazazi wake na mtu anayemsaidia ni mwanaye wa kiume
anayeitwa Wambura Juma aliyekuwa akisoma kidato cha tano.
“Mtoto
wangu huyu kwa sasa hasomi kwa sababu ya kunisaidia mimi, alilazimika
kuacha masomo toka tukio hili liliponitokea,” alisema Neema.
ANA MIEZI NANE HOSPITALINI
Neema
anasema tangu alazwe hospitalini hapo, sasa ni mwezi wa nane lakini
anamshukuru Mungu ameanza kujikongoja kutembea japo kwa taabu sana.
Muonekano wa jeraha alolipata Neema baada ya kuunguzwa na mumewe kwa uji wamoto.
MADHARA ALIYOYAPATA
Neema
amepata madhara makubwa kufuatia tukio hilo kwani kwa sasa mkono wa
kulia haukunjuki sawasawa kama zamani, hawezi kunyoosha shingo kutokana
na nyama za shingo kuungana na kidevu, mdomo wake umepinda kidogo huku
titi la upande wa kulia likiwa halipo tena!
APATIWA SIMU YA MKONONI
Joyce
Kiria ni Mtangazaji wa Kipindi cha Wanawake Live kinachorushwa hewani
na Runinga ya EATV, alimtembelea Neema hospitalini na kumpa msaada wa
simu ya mkononi ili iwe rahisi kwa wale watakaojitokeza kutaka kumsaidia
kwa ajili ya pesa za matibabu kutumia simu hiyo.
ANAHITAJI MSAADA
Ndugu
msomaji, Neema anahitaji msaada wako wa hali na mali. Kama utakuwa na
chochote na umeguswa na maumivu yake, unaombwa kutumia mawasiliano yake
0656 151 072 au 0756 768 305.
0 Comments