MAAJABU! Mtoto Irene
Emmanuel Joseph (1) mkazi wa Kibamba-Mji Mpya jijini Dar, ameendelea
kuwa gumzo kufuatia kufariki dunia Agosti, mwaka jana akiwa na miezi 9
na kudaiwa kufufuka katika mazingira ya ajabu hivi karibuni akiwa na
umri wa mwaka mmoja na miezi minne, Uwazi linakuletea.
Mtoto Irene Emmanuel Joseph baada ya kufufuka.
UWAZI KAMA KAWAIDA YAKE
Tukio la kupatikana kwa
mtoto huyo akiwa hai lilitikisa Jiji la Dar, Jumamosi iliyopita ambapo
umati ulifika nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo ili kumshuhudia kwa
macho.
Kama ilivyo ada, Gazeti
la Uwazi ni kuchimba kwa kina matukio yenye kuishangaza na kuisikitisha
jamii. Nalo lilifika nyumbani hapo kwa lengo la kukusanya taarifa kwa
undani ili kuwapelekea wasomaji wake.
MAZINGIRA YA KIFO CHAKE
Akizungumza na gazeti
hili nyumbani hapo, mama mzazi wa mtoto huyo, Helena Raphael alisema
kuwa, ilikuwa Agosti mwaka jana akiwa kwenye eneo la biashara yake,
Mbezi Mwisho, Dar, Irene aliugua ghafla. Alionesha kulegea na kuwa kama
mtoto mwenye degedege.
“Nilimwambia mume wangu,
tukampeleka kwenye zahanati moja iliyopo palepale Mbezi ambapo daktari
akabaini kuwa tatizo la mwanangu ni kubwa hivyo akatushauri tumkimbize
Hospitali ya Tumbi, Kibaha, Pwani ambapo iligundulika kwamba alikuwa na
upungufu mkubwa wa damu.
“Pale hospitali
madaktari walianza kutafuta mishipa ili wamchome kwa lengo la
kumwongezea damu lakini cha ajabu mishipa ya mwanangu ikawa inavimba tu.
Ilipofika saa 6 usiku, alifariki dunia bila kuwekewa damu. Nililia sana
kama mzazi!”
Irene Emmanuel akiwa na baba'ke.
MAITI YAMDUWAZA MAMA MTU
“Baada ya kifo, sikuwahi
kuuona mwili wa mwanangu maana waliupeleka mochwari. Siku ya kuaga
mwili hapa nyumbani kwa ajili ya mazishi, nilishangaa sana kumwona
mwanangu ana alama ya duara kwenye shavu kama zile alama za Wamasai.
“Niliwasimulia baadhi ya
waombolezaji wakasema kwa upande wao waliuona mwili wa mwanangu ukitoka
jasho jingi kama mtu aliyetoka kufanya kazi ngumu juani na ulivimba
sana,” alisimulia mama huyo na kuongeza:
“Pamoja na hayo, tulimzika mwanangu kwenye makaburi yaliyopo hapahapa Mji Mpya huku tukiwa na shaka juu ya kifo chake.”
MAMA AANZA KUZUNGUKA MAKANISANI
Helena anasema baada ya
mazishi, alianza kwenda kwenye makanisa mbalimbali kumwomba Mungu
amrejeshe mwanaye na mwishowe akajikuta amefika kwenye kanisa la Nabii
Flora lililopo Salasala, Dar ambako aliambiwa mtoto wake alikuwa hai.
“Nilikuwa naenda kusali
kila siku ndipo siku moja Nabii Flora alinifuata na kuniambia mwanangu
hajafa alikuwa yupo sehemu lakini nguvu zake haziwezi kumrudisha tena.
Irine siku chache kabla hajafariki.
MGANGA ADAI AMEMPATA MTOTO
“Siku ya kwanza kumpigia
simu huyo mganga alituambia tushike shilingi mia moja mkononi,
tukafanya hivyo, akasema kweli mtoto wetu yupo hai na atamrudisha. Siku
chache mbele tulimtumia hela alizotuagiza na akatuambia tusafiri kwenda
Dodoma tukamchukue mtoto wetu kwani tayari alishampata.”
WAZAZI WAONANA NA MTOTO
Helena anasema kuwa,
Februari mwaka huu yeye na mume wake walisafiri mpaka Dodoma eneo la
Pandambili na kuonana na mganga huyo akiwa na mtoto wao ambaye
alionekana kutokuwa na afya nzuri. Walitakiwa wamuache kwa muda ili
aendelee na matibabu mpaka arejee kwenye hali ya kawaida.
MGANGA ATINGA DAR NA MTOTO
“Baada ya miezi miwili
kupita mganga alitutaarifu kuwa anakuja Dar na mtoto. Kweli, alifika
hapa usiku wa Aprili 10 akiwa na mtoto wetu ambaye kwa sasa ni mzima
kabisa.
“Tuna furaha sana
kuonana na mwanetu tena haya kweli ni maajabu ndiyo maana watu wengi
wamefika hapa kushuhudia na wengine wamelala hapahapa tangu jana,”
alisema mama huyo.
Hili ni kaburi la mtoto Iline.
MGANGA ANENA
Naye mganga aliyedai
kumfufua mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina la Bino alikiri kupokea
simu kutoka kwa wazazi hao na kusema:
“Niliongea na mizimu
ikaniambia mtoto yupo hai katika mazingira ya kawaida ila alichezewa
kimazingara. Nimewasaidia wengi tu na ninao watu wengi niliowarudisha
huko Dodoma,” alisema mganga huyo.
MJUMBE ATHIBITISHA KUZIKWA KWA MTOTO HUYO
Mjumbe wa mtaa huo,
Maimuna Abdallah alithibitisha kupokea taarifa ya kifo cha mtoto Irene,
Agosti mwaka jana na kuongeza kuwa yeye ndiye aliyetoa barua ya
utambulisho wa makazi kwa baba mzazi wa mtoto huyo ili aweze kupatiwa
mwili wa mwanaye kutoka Hospitali ya Tumbi kwa ajili ya mazishi.
“Na mimi nimeshangazwa
sana na tukio hili kwa sababu tangu nizaliwe sijawahi kusikia wala kuona
mambo haya, niwaambieni tu kuwa kweli yametokea mtaani kwangu,” alisema
mjumbe huyo.
MAJIRANI WAO
Baadhi ya majirani na
wazazi wa Irene waliliambia Uwazi kwamba, japokuwa mtoto huyo alifariki
dunia mwaka jana na kuzikwa lakini walivyomwona wao ni yeye yule
waliyemzika!
“Yaani hakuna shaka
kabisa kwamba huyo mtoto ni Irene mwenyewe, sijui nini kilifanyika
lakini kusema kweli ni mwenyewe na kweli kifo chake kiliacha maswali
hapa mtaani,” alisema jirani mmoja.
Majirani wakiwa kwenye tukio hilo.
UWAZI LATINGA KABURINI
Ili kuthibitisha kuzikwa
kwa mtoto huyo, gazeti hili lilifika kwenye kaburi alilozikwa mtoto
Irene mwaka jana na kulikuta limeshaota majani huku mchwa wakiwa
wameanza kuutafuna msalaba sehemu ya chini.
Msalaba huo ulisomeka hivi; IRENE EMMANUEL, KUZALIWA 01/10/2013. Hata hivyo, sehemu yenye tarehe ya kifo ndiyo ililiwa na mchwa.
MPANGO WA KULIFUKUA KABURI
Baba mzazi wa Irene alipoulizwa kama wana mpango wa kulifukua kaburi alilozikwa binti yake, alisema hawajafikiria hilo.
KWA SASA IRENE
Kwa sasa, mtoto Irene
yuko kwa wazazi wake huku mganga huyo akisema ataendelea kumpatia dawa
mpaka atakapoimarika zaidi na kuendelea na makuzi.
0 Comments