Wakati Mbunge wa Arumeru
Mashariki, Joshua Nassari akisema anashindwa kuamini kilichotokea na
kunusurika katika ajali ya helikopta juzi, mmiliki wa chopa hiyo,
Philemon Ndesamburo amesema atanunua nyingine haraka kabla ya kuanza
kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Kauli hizo zilitolewa
jana ikiwa ni siku moja baada ya helikopta hiyo inayomilikiwa na
Ndesamburo kupitia kampuni yake ya Keys Aviation kupata ajali wakati
ikitumiwa na Nassari na baadhi ya viongozi wa Chadema.
Wakati ikipata ajali, ilikuwa imekodishwa na Kampuni ya General Aviation Services (T) Ltd inayomilikiwa na Kapteni William Slaa.
Katibu wa Ndesamburo,
Basil Lema alisema ilipata ajali baada ya kupigwa na kimbunga wakati
anga likiwa limefunikiwa na wingu zito.
“Mheshimiwa Ndesamburo
amemshukuru Mungu kwa kuwanusuru watu waliokuwa kwenye ndege hiyo ambao
ni pamoja na Mbunge Joshua Nassari.
“Ameweka wazi kwamba
atalazimika kununua nyingine mapema kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye
kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka huu,” alisema Lema akimnukuu Ndesamburo.
Lema alisema rubani
aliyekuwa akiendesha helikopta hiyo alifanikiwa kuielekeza juu ya miti
alioutumia kupunguza kasi ya kushuka chini na kusaidia abiria kutoka
salama.
“Imeharibika lakini
abiria wote ni wazima. Walikuwamo wanne,” alisema na kuongeza kuwa
helikopta hiyo ndiyo iliyotumiwa na Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa 2010
na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka jana na chama hicho kilitegemea
kuitumia katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Pia, imewahi kutumiwa na
makada mbalimbali wa CCM akiwamo Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu
Nchemba na kada maarufu wa Moshi mjini, Buni Ramole.
Kauli ya Nassari
Akizungumza na waandishi
wa habari katika wodi alikolazwa kwenye Hospitali ya Seliani – Arusha,
Nassari alisema waliporuka kutoka Leguruki, hakukuwa na dalili zozote za
kuchafuka kwa hali ya hewa, lakini dakika chache baada ya kuruka angani
wingu zito lililoambatana na upepo mkali liliwafunika ghafla.
“Wingu lile na upepo ule
sijawahi kuona katika maisha yangu yote zaidi ya kusoma kwenye vitabu
vya simulizi vya mambo ya ushirikina. Namshukuru Mungu wote tuko salama
kwani hatukuwa na matumaini ya kupona ajali ile,” alisema Nassari.
Mbunge huyo aliyekuwa
katika ziara ya kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwenye Daftari la
Wapigakura, alimwagia sifa rubani Slaa kwa uwezo na ustadi aliouonyesha
hadi wakanusurika.
“Kama siyo ustadi wake,
naamini watu wangeokota vipande vya nyama tu kwenye eneo la ajali, ila
Mungu ni mkuu leo tuko hai wote licha ya madhara madogo,” alisema.
Nassari alisema muda
mfupi kabla ya kuruka saa kumi na moja jioni, wakati akihutubia mkutano
huko Leguruki, alipokea simu kutoka kwa mchungaji mmoja akimtaarifu
kupata maono kuwa anakabiliwa na hatari ya kukutwa na jambo kubwa na
baya akimtaka adumu katika sala.
“Dakika 15 baadaye
nikaruka na kupata ajali. Naamini kilichotuokoa ni nguvu ya sala
niliyosali baada ya kupokea ujumbe wa mchungaji na maombi ya wachungaji
wangu wanaoniombea kila siku,” alidai Nassari.
Rubani Slaa alisema
alishangaa lilipotokea wingu na upepo uliosababisha ndege kuanguka ikiwa
njiani kuelekea Ndoombo na Ngureserosambu.
“Kabla ya kurusha ndege
nilijiridhisha na hali ya hewa. Hakukuwa na kiashiria chochote cha hali
ya hatari kama maeneo mengine ambako tulishindwa kutua kutokana na mvua
zilizokuwa zikinyesha."
Kaimu Mkurugenzi wa
Hospitali ya Seliani, Dk Paul Kisanga alisema hali za majeruhi si mbaya,
isipokuwa Eva Kayaha aliyevunjika mbavu mbili.
0 Comments