Advertisement

Responsive Advertisement

Wabunge Wagonga Mwamba Kwa Rais Magufuli......Agoma Kuwaongoza Hela Ya Posho,Apunguza Mikopo Ya Mashangingi


Wakati Serikali ikihaha kutafuta fedha kwa ajili ya kuendeshea shughuli zake, wabunge wameingia kwenye mvutano na ofisi ya Bunge kuhusu fedha ambazo  wanastahili kupewa kwa ajili ya kununulia magari yao.

Mwaka 2010, wabunge walilipwa Sh90 milioni kwa ajili ya ununuzi wa magari hayo aina ya Toyota Land Cruiser (hardtop), ambayo ni vitendea kazi vyao. Wabunge hutakiwa kulipa nusu ya fedha hizo wkati nyingine ni mchango wa Serikali.

Lakini wakati gharama za maisha zikipanda huku thamani ya Shilingi ikiporomoka kulinganisha na Dola ya Marekani na hivyo kusababisha bidhaa kupanda bei, wabunge wamekataa kulipwa kiasi hicho cha fedha mwaka huu na badala yake wanataka walipwe kulingana na bei ya sokoni ya magari aina hiyo.

Wabunge wanataka walipwe Sh130 milioni ambazo wanasema ni bei ya magari hayo kwa sasa baada ya kupanda bei. Hata hivyo ombi  hilo  limegonga  mwamba

Wakizungumza  kwa sharti la kutotajwa majina, baadhi ya wabunge walisema mara baada ya kujisajili bungeni kwa ajili ya uzinduzi wa Bunge la Kumi na Moja, katibu wa chombo hicho, Dk Thomas Kashililah alifanya kikao na wabunge wote ili kuwapa taratibu lakini pia kuwafahamisha stahili wanazopaswa kupata kama wabunge.

“Katibu alitujulisha kuwa hakuna ongezeko lolote la posho, hivyo  tunapaswa kulipwa kiasi kilekile cha Sh300,000 kwa siku .
 
"Lakini pia alisema tutapewa Sh90 milioni kwa ajili ya mkopo wa gari badala  ya  milioni 120 ,” alisema mmoja wa wabunge hao.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, suala hilo liliibua mjadala na kusababisha wabunge kuhoji iweje kiwango hicho kitumike katika Bunge la Kumi na Moja, miaka mitano baada ya wabunge wa Bunge la 10 kupewa kiasi hicho.

“Unajua magari tunayotakiwa kununua ni Toyota Land Cruiser Hardtop, na ukweli sasa thamani ya magari hayo imepanda sana huwezi kuifananisha na mwaka 2010 wakati wa Bunge la 10,” alisema mbunge mmoja.

Wabunge hao walitaka walipwe kiasi cha Sh130 milioni kwa madai kuwa ndiyo bei ya sokoni ya magari aina hiyo.

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Anatropia Theonest amesema hawajakataa fedha hizo, lakini thamani ya Dola imepanda hivyo kusababisha thamani ya magari hayo kupanda pia.

“Hakuna asiyejua kwamba thamani ya Dola imepanda na kwa kawaida kila Bunge kunakuwa na ongezeko la Sh30 milioni. Mfano Bunge la Tisa walipewa Sh60milioni la 10 wakapewa Sh90milioni, hivyo ilipaswa sasa iwe Sh 120mililioni ili kuendana na soko,” alisema mbunge huyo.

Akizungumzia sakata hilo,naibu katibu wa Bunge, John Joel alisema jukumu la ununuzi wa magari ya wabunge, lipo chini ya Serikali na siyo ofisi yake hivyo ni bora wangeulizwa wenye jukumu hilo.

“Tunachofamu sisi mbunge anatakiwa apewe vitendea kazi likiwemo gari, lakini wanaohusika na hilo ni Serikali,” alisema.

Alisema ofisi ya Bunge hushauriana na Serikali namna ya kutoa huduma kwa wabunge na kwamba kwa jinsi anavyofahamu, mpaka jana watunga sheria hao walikuwa hawajapewa fedha yoyote ya kununua magari kwa awamu hii, hivyo wanasubiri utaratibu.

Wakati Joel akisema Serikali ndiyo inahusika, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue aliurudisha mpira kwenye ofisi hiyo ya Bunge, akisema uongozi wa bunge umekwisha pewa maelekezo yote na serikali  juu  ya  ununuzi  wa  magari hayo, hivyo akamtaka mwandishi akawaulize wao ( uongozi wa bunge)

Katika kukusanya fedha za kuwezesha kutekeleza mipango ya Serikali na ahadi alizotoa wakati wa kampeni, Rais John Maguguli alitangaza hatua mbalimbali za kudhibiti matumizi, na akawaeleza wabunge mwishoni mwa wiki kuwa hataweza kufanikiwa iwapo hatapata ushirikiano wao.

Katika kuonyesha kuwa anatoa kauli thabiti, Dk Magufuli aliagiza fedha ambazo zilichangwa na taasisi mbalimbali za fedha kwa ajili ya hafla za kuwapongeza wabunge, zielekezwe kwenye ununuzi wa vifaa tiba kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Tayari Rais ameshafuta safari za nje isipokuwa kwa kibali cha Ikulu baada ya mtu anayetaka kusafiri kutimiza masharti kadhaa, likiwamo linalomtaka aeleze faida ya safari yake na kama iwapo hatasafiri, nchi itaathirika vipi.
Mpekuzi blog

Post a Comment

0 Comments