Dar es Salaam, Tanzania. Baada ya miaka 13 ya kuwapo
katika fani ya sanaa ya maigizo, hakuna shaka kwamba, Steven Jacob
maarufu kama JB, kwa sasa ni miongoni mwa watu wenye majina makubwa mno
katika fani hiyo nchini.
Ni miongoni mwa nyota `Watano’ Bora zaidi wa
kiume kwa upande wa fani hiyo, hivyo kumfanya kuwa katika hadhi ya juu,
sawa na nyota wengine kama akina Steven Kanumba na Vincent Kigosi `Ray’
na wengine.
Ndiyo maana haishangazi kuona kwamba, hata leo hii ukiingia katika soko la filamu zilizo juu, huwezi kukosa kazi za nyota huyo. Kwa sasa, JB, mtu mwenye umbo la miraba minne licha ya kucheza
filamu ni mwandishi wa filamu na mtayarishaji, anatamba na ‘Illegal
Sisters’, ‘Signature’, ‘Tanzanite’ na ‘Msamaha wa Rais’, Nakwenda kwa
mwanagu, Dereva tax D.N.A na nyingine nyingi. Katika mahojiano
na tovuti hii hivi karibuni, JB anasema kwamba, ana kila sababu ya
kujivunia mafanikio yake, ingawa hawezi kuvimba kichwa kwa umaarufu,
huku akisisitiza alianza kuigiza kama mzaha na baadaye taratibu fani
ikamkolea na kuigeuza sehemu ya maisha yake. Anasema kwamba, alikuwa `anaburuzwa’ na rafiki yake, Single
Mtambalike ‘Richie Richie’ ajiunge na kundi lao la wasanii wanne
lililoitwa Four For You ambalo mbali ya Richie, wengine walikuwa Anna
Costantine `Waridi’, Allen Raymond `Bishanga’ na Aisha. “Kwa kuwa tulikuwa pamoja muda mrefu katika maskani pale Sinza
Kijiweni, nilihisi kama nabughudhiwa, nikawa nakwenda mazoezini kila
jioni, ingawa wakati mwingine nilikuwa nawakimbia,” anasema JB
akisimulia alivyoingia kwenye maigizo na baadaye filamu mwaka 1997. Mwaka mmoja baadaye, yaani mwaka 1998, akajiunga na kundi hilo
rasmi ili kumfurahisha Richie na mwaka 1999 kundi hilo lilitoa mchezo,
`Kuvuja kwa mitihani.’ Anasema katika zoezi la kuboresha kundi
waliwaongeza wasanii, kama Suzane Lewis `Natasha’ na mwanawe Yvonne
Cherie `Monalisa’. Aliongezeka pia George Otieno `Tyson’ ambaye baadaye alimuoa
Monalisa. Kutokana na kukua kwa kundi hilo, walilibatiza Nyota
Enssemble. Baada ya kuvuma kwa mchezo wa kwanza, akaja kupata moyo
kutokana na mchezo wa ‘Nyota’ ambao ulikuwa mrefu kuliko wote nchini. Alizidi kuipenda sanaa hasa baada ya kupata hamasa kutoka kwa
wasanii wa mchezo wa Tausi, kutoka Kenya Kibibi na Dama walipoigiza
sehemu ya igizo hilo. Akajiuliza juu ya maswali mengi kwanini wenzao
waweze wao washindwe , na ndipo akajikuta akiongeza juhudi ingawa kwa
kiasi kidogo sana. Sifa kwa wasanii zikaanza kupanda, na kila mmoja kujiona anaweza
kufanya zaidi ya mwenzake, kulipelekea mwaka 2002 Nyota Enssemble
likajigawa na kutokea kundi lingine lililojulikana kama Nyota Academia.
Katika kundi la Nyota Academia walitoka Monalisa, Natasha, Tyson, kwa
kuwa JB, sanaa aliifanya kwa kumfuata Richie Richie, ikambidi ahame
kumfuata alipo. Nyota Anssemble ITV, ikabakiwa na Bishanga, Aisha, Waridi, Seki
na wasanii wengine wachanga . Walipata nafasi CTN, na huko waliweza
kuongeza wasanii wengine kama Vicent Kigosi `Ray’, Ben Kinyaiya, Macha
na wengine ambao kwa pamoja walifyatua igizo moja la ‘Suzi’ na baada ya
hapo walifanya igizo la mwisho na kundi likavunjika. Baada ya kutamba katika maigizo, ndipo mwaka 2003 akageukia
filamu, akiicheza kwa mara ya kwanza katika filamu ya `Masaa 24’.
Kuanzia hapo aliunganisha filamu moja hadi nyingine, huku akijizolea
umaarufu kila kukicha. Na haikushangaza kuona akichaguliwa kuwa Mwigizaji Bora wa Kiume
nchini katika tuzo za Vinara mwaka 2008. Kutokana na kuiva katika
filamu, akaona sasa inatosha na hivyo kufikia kuanzisha kampuni yake. Ndoto yake ilitimia mwaka 2005 baada ya kuanzisha kampuni
aliyoiita Jerusalem. Hata hivyo, ilikuwa `mbinde’ kuanzisha Jerusalem,
kwani hakuwa na fedha, hadi alipobebwa na Mohammed Mpakanjia
`Kitendawili’ ambaye kwa sasa ni marehemu aliyempatia Sh milioni 1.5,
huku Fujo naye akitoa kiasi kama hicho na hivyo kuanzisha rasmi
kampuni. Filamu ya kwanza ikawa `Kanisa la Leo’ mwaka huo huo wa 2005.
Hata hivyo, Fujo alijitoa, hivyo kumlazimu JB kumtafuta mbia mwingine na
kufanikiwa kumnasa swahiba wake, Richie Richie. Walitengeneza filamu za
‘Agano la Urithi’, `Stranger’, `Swahiba’ na `Kwa Heshima ya Penzi’.
Baada ya filamu hizo, Richie naye akaachia ngazi na kuanzisha kampuni
yake, Bulls Entertainment. JB hakutetereka, bali aliimarisha zaidi kazi yake na kufyatua
filamu nyingi zikiwamo Regina, My Fiance, Born Again, 14 Days, Signature
na hivi karibuni anatarajia kuizindua filamu ya Zawadi ya Birthday
aliyomshirikisha Richie. Lakini nje ya filamu, JB ni Mwinjilisti na mfanyabiashara
`mchakarikaji’ kweli kweli. Na hakuanza jana au leo, bali siku nyingi
wakati huo akichukua mahindi mikoani na kuyauza Dar es Salaam. Biashara
yake ilikua na kufikia hatua ya kumiliki kampuni ya usagishaji wa
nafaka, akiagiza mahindi na kuuza unga kwa kutumia nembo ya `Sembe
Mama’. Kama si uzembe wake, hakika JB leo hii asingevuma kama msanii
mahiri wa maigizo, bali kama mfanyabiashara mashuhuri kutokana na
biashara zake kumwendea vyema tangu alipozianzisha mwaka 1996. Ni uzembe
gani alioufanya JB? Mwenyewe hafichi, anasema kamari ndiyo iliyozamisha
mtaji wangu na kumrudisha chini kabisa. Katika hilo, mpaka leo
anajutia uamuzi wake wa kuukumbatia mchezo huo, ambao anasema kwa siku
ulikuwa `unamla’ kati ya sh laki mbili na wakati mwingine kufikia hata
sh milioni mbili. “Kamari imenifilisi sana na kunirudisha nyuma kimaisha.Kwa siku
nilikuwa nacheza hata katika baa 15 hadi 20 bila kujua kuwa nilikuwa
najiumiza mwenyewe. “Kutokana na uchezaji mkubwa wa kamari niliitwa jina
la Binkololo, sababu ya yale makamari yalikuwa yakilia hivyo endapo mtu
ukishinda. Marehemu Mpakanjia alinisihi niachane na kamari, lakini
haikuwezekana hadi siku moja nilipoliwa fedha nyingi.” Anakumbuka
kwamba, siku hiyo alijiinamia, akatokea mzee asiyemjua na kumwambia,
“Bora kamari ingekuwa inakula fedha zako, lakini inakuongezea nuksi
katika maisha yako.” Maneno hayo yalimuingia vizuri na kuanzia hapo
aliamua kuipa kisogo kamari. Mbali ya kamari, sababu nyingine iliyomfilisi ni baadhi ya
wateja wake wa mahindi kushindwa kulipa madeni, huku baadhi yao
wakikimbia na fedha zake. Lakini baada ya misukosuko ya kibiashara, na
kupata ujasiri akiwa katika ulimwengu wa maigizo na filamu, anasema sasa
ana mengi ya kujivunia hasa Kampuni yake ya Jerusalem. Anasema
mbali ya mafanikio ya kazi za kisanii na kiuchumi, pia anajivunia
kampuni yake kuwaibua wakali wa filamu kama Rose Ndauka, Elizabeth
Kiyumba ’Nikita’, Steve wa Maisha Plus, Brigit mtangazaji wa EA TV, Lady
Anifa na wengine. Anasema Kampuni ya Jerusalem imemwezesha kufungua maduka jijini
Dar es Salaam na kwamba sasa anajipanga kuifufua tena kampuni yake ya
kusaga nafaka. “Na zaidi ya yote ni umaarufu na shughuli zangu
zinaniwezesha kukidhi mahitaji yake yote ya msingi,” anasema JB ambaye
anasema kwa sasa yeye ni mhubiri wa masuala ya dini na kwamba hata
filamu zake zimeegemea katika upande wa dini, hasa ya Kikristo. Akifafanua kuhusu `ulokole’ wake, anasema wakati wa kuigiza
haimzuii kuingia mahali panapokwenda kinyume na imani za dini yake kwa
sababu dhamira inakuwa kupata mazingira halisi ya sehemu anayoigiza. Anakiri kwamba, hali hiyo si kwamba inawashangaza watu wa nje ya
fani na familia yake, bali hata mkewe akidai haamini kama anaweza
kushinda baa, klabu na sehemu nyingine bila ya kwenda kinyume cha imani
yake. “Wakati mwingine mke wangu anakosa, lakini kama ni mazingira
fulani basi nafanya hivyo ili kuiga uhalisia wa filamu ninayoicheza,”
anasema anayewahusudu kisanii Single Mtambalike kwa hapa Tanzania na
Amitabh Bachan, gwiji wa filamu wa India tangu miaka ya 1970 ambaye
katikati ya miaka ya 1980 alikuwa Mbunge nchini mwake. Anamhusudu pia mwanamuziki na mwigizaji wa Marekani, Jeniffer
Lopez `J.Lo’. Kwa upande wa filamu zake, anakiri Regina ndiyo
anayoihusudu mno. “Niseme tu kwamba, ili kuiimarisha zaidi kampuni
yangu, mwaka huu utakuwa wa mwisho kucheza filamu zitakazoandaliwa nje
ya kampuni yangu kwa sababu naamini nina uwezo wa kufanya mambo makubwa
nikiwa na Jerusalem,” anasema JB ambaye pia ni mkali katika mchezo wa
soka akiwa sentahafu. Makali yake aliyaonesha akiwa kambi ya JKT Mgambo mkoani Tanga
alikokutana na Ramadhani Nassib, Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF). Mtaani, aliichezea timu Mutukuru ya Mwananyamala,
jijini Dar es Salaam akiwa na makipa maarufu waliowahi kuzichezea Simba,
Yanga na Taifa Stars, Joseph Fungo na Joseph Katuba ambaye kwa sasa ni
marehemu. Kwa upande wa elimu, alisoma Shule ya Msingi
Forodhani alikohitimu mwaka 1984 na baadaye kujiunga na Sekondari ya
Popatlal ya Tanga hadi mwaka 1988 na baadaye kidato cha tano na sita
alikozamia katika masomo ya Uchumi na Biashara. Kutoka hapo
akaangukia JKT kwa mwaka mmoja. Huyo ndiye Jacob Steven ambaye
hajabahatika kupata mtoto, kwani ndoa yake ndiyo
0 Comments