SERIKALI imepanga kutumia Sh trilioni 19. 7 katika mwaka wa fedha
2014/2015, kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo, tofauti na Sh
trilioni 18.2 ya mwaka huu wa fedha unaoishia Juni 30.
Katika fedha hizo, matumizi ya kawaida yamepangwa kuwa Sh trilioni
14.2, ambapo kati ya hizo Sh trilioni 5.1 ni kwa ajili ya mishahara ya
watumishi wa Serikali, taasisi na wakala wake.
Aidha Sh trilioni 4.4 zimetengwa kwa ajili ya Mfuko Mkuu wa Serikali
na Sh trilioni 4.4 kwa ajili ya matumizi mengine. Waziri wa Fedha, Saada
Salum Mkuya alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akiwasilisha Mpango
wa Bajeti ya mwaka ujao wa fedha kwa wabunge.
*Matumizi ya Maendeleo
Alisema makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa mwaka ujao wa fedha ni
Sh trilioni 7.7 sawa na asilimia 39.3 ya matumizi yote ya Serikali na
kati ya kiasi hicho, miradi ya maendeleo imetengewa Sh trilioni 5.4 sawa
na asilimia 27.7 ya matumizi yote ya Serikali, huku matumizi mengine ya
maendeleo yakitengewa Sh trilioni 2.2.
“Kwa upande wa matumzi mengine ya maendeleo, a s i limia 63 inagharimiwa na fedha za ndani hivyo kuongeza kujitegemea,” alisema.
Alisema katika matumizi mengine ya maendeleo Sh bilioni 751.7
zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara, Sh trilioni 1.4
zimetengwa kwa ajili ya malipo ya mikopo iliyokopwa na makusanyo ya
Halmashauri ya Sh bilioni 138.7, yatatumika kwa ajili ya maendeleo.
Vipaumbele
Kwa mujibu wa Waziri Mkuya, katika matumizi ya maendeleo, Bajeti
itazingatia kutekeleza Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini
(Mkukuta II), Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano 2011/2012 mpaka
2015/2016 na Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Katika BRN, Waziri Mkuya alisema Bajeti itajielekeza katika maeneo
sita ya kitaifa ambayo ni kilimo, elimu, maji, utafutaji rasilimali
fedha, nishati na uchukuzi na uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji
biashara.
Kilimo
Katika Kilimo, Serikali inapanga kuhamasisha kilimo cha kibiashara
cha ngano na miwa ya kuzalisha sukari katika Mto Wami, Ruvu, Kagera,
Kilombero na Malagarasi.
Pia inalenga kuboresha skimu za masoko na umwagiliaji wa mpunga kwa
ajili ya wakulima wadogo, kujenga skimu za pamoja kwa ajili ya
kuwaunganisha wakulima wa mahindi na masoko na kuongeza upatikanaji na
utumiaji wa pembejeo, zana za kilimo na huduma za ugani.
Elimu Serikali katika elimu, imepanga kuweka mkazo katika maeneo
yaliyokubaliwa kutekelezwa chini ya BRN, ambayo hata hivyo
hayakufafanuliwa.
Maji Waziri Mkuya alisema katika sekta ya maji, Serikali inapanga
kuwezesha kudumu kwa miradi iliyopo ya maji kwa kuhakikisha jamii
inashirikishwa ipasavyo katika kuisimamia.
Pia Serikali imepanga kuongeza vituo vya upatikanaji maji vijijini
kwa kupanua, kukarabati pamoja na kujenga vituo vipya vya usambazaji
maji.
Malengo mengine ya kipaumbele ni kuendelea na utekelezaji wa miradi
ya kimkakati ya maji ikiwa ni pamoja na Kimbiji, Mpera na bwawa la
Kidunda na kuboresha miradi ya usambazaji maji safi na taka katika
maeneo ya mijini.
Madini
Katika sekta ya madini, msisitizo uliwekwa katika kuhakikisha
Serikali inapata mapato ya kutosha kutoka sekta ya madini kwa kuzijengea
uwezo ofisi za kanda na kuhamasisha uongezwaji wa thamani wa madini ili
kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Miundombinu
Sekta ya miundombinu katika malengo hayo ya kipaumbele, imegawanywa
katika makundi sita ambayo ni reli, barabara, madaraja na maghati,
bandari na usafiri wa majini, usafiri wa anga, utabiri wa hali ya hewa
na nishati.
Katika nishati, Serikali imelenga kukamilisha ujenzi wa bomba la gesi
asilia kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam na kuendeleza
utekelezaji wa miradi mingine 28 ya umeme chini ya mfumo wa BRN.
Pia Serikali imelenga kuendelea kuimarisha miundombinu ya uzalishaji
nishati ya umeme iliyopo pamoja na kupeleka umeme vijijini na
kuhamasisha uwekezaji katika nishati jadidifu.
Katika eneo hilo la miundombinu, Serikali imejipanga kuboresha
miundombinu ya utabiri wa hali ya hewa pamoja na kujenga uwezo wa
watumishi na taasisi ya utabiri wa hali ya hewa.
Katika eneo la usafiri wa anga, Serikali imepanga kuboresha
miundombinu ya usafiri wa anga, kujenga viwanja vya ndege katika maeneo
ya kimkakati pamoja na kukarabati vilivyopo na kuboresha mazingira ya
kibiashara ilikuvutia wawekezaji.
Reli, barabara, bandari
Kuhusu reli, Serikali imejipanga kuweka mkazo katika kuendelea
kuimarisha Reli ya Kati, kukarabati na kutengeneza reli zilizopo,
ununuzi wa vichwa vya treni, mabehewa na vifaa vingine.
Pia Serikali imejipanga kukarabati na kutengeneza mifumo ya
mawasiliano ya simu pamoja na mfumo wa ufuatiliaji wa mizigo na
kuendelea na utekelezaji wa miradi mipya ya reli katika maeneo ya
kimkakati.
Kwa upande wa barabara, Serikali imejipanga kujenga na kukarabati
barabara zinazofungua fursa za kiuchumi pamoja na kupunguza foleni
katika maeneo ya mijini, kujenga na kuimarisha mizani, kutekeleza miradi
mingine 23 ya barabara iliyoainishwa chini ya mfumo wa BRN na
kuendeleza na kuimarisha barabara zinazounganisha mikoa, wilaya na
vijiji, kujenga madaraja, maghati na ununuzi wa vivuko.
Katika bandari, Serikali imejielekeza kujenga bandari mpya katika
maeneo ya kimkakati pamoja na kuimarisha zilizopo, kuongeza uwezo wa
kubeba mizigo katika bahari, maziwa na bandari kavu na kuongeza ufanisi
wa utendaji kazi katika bandari na kuweka mazingira stahiki kwa ajili ya
sekta binafsi kuwekeza.
Kipaumbele cha sita katika mfumo wa BRN, kitakachozingatiwa na Bajeti
ijayo, ni utafutaji wa rasilimali fedha, ambapo Serikali imejipanga
kupanua wigo wa ukusanyaji kodi ikiwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji
wa ushuru wa forodha.
Pia Serikali imejielekeza kuimarisha ukusanyaji wa mapato yasiyo ya
kodi, kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya ubia kati ya Serikali na
sekta binafsi, pamoja na kuanzisha mfuko maalumu kwa ajili ya kuwezesha
ubia kati ya serikali na sekta binafsi.
Serikali pia imejipanga kuanzisha mfuko maalumu kwa ajili ya
kuwezesha ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, kuhimiza malipo kwa
njia ya mtandao na kupunguza misamaha ya kodi.
Mapato
Waziri Mkuya alisema sera ya mapato kwa mwaka 2014/2015, inalenga
kuimarisha utaratibu wa kukusanya mapato pamoja na kudhibiti na
kupunguza misamaha ya kodi hadi asilimia moja ya Pato la Taifa.
Serikali pia imepanga kukamilisha utungwaji wa sheria ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT), kuongeza wigo wa kodi kwa kuimarisha vyanzo
vilivyopo na kuainisha vyanzo vipya pamoja na kurasimisha sekta isiyo
rasmi, ili iingie kwenye mfumo rasmi wa kodi.
“Serikali imekamilisha utafiti wa mfumo wa ukusanyaji wa mapato
yasiyo ya kodi ambapo utafiti umelenga kuhuisha na kuwianisha mifumo ya
ukusanyaji wa mapato hayo ambapo matokeo yake yatajumuishwa katika
maboresho ya mfumo wa kodi kwa mwaka huu,” alisema.
0 Comments