Rais Jakaya Kikwete ametoa ahadi mbili za kuwafurahisha
wafanyakazi. Kwanza ametangaza nia ya kuongeza mishahara yao na pili,
kupunguza kodi inayokatwa kwenye mishahara hiyo mambo ambayo ameahidi
kutekelezwa katika Bajeti ya mwaka 2014/2015 inayotarajiwa kuwasilishwa
bungeni hivi karibuni.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi), yaliyofanyika kitaifa Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema anatambua kuwa wafanyakazi wana hamu ya kujua Serikali itasema nini kuhusu masilahi yao.
Alisema malalamiko ya wafanyakazi wengi ni kutaka
kuona kima cha chini cha mshahara kinaongezwa huku kodi kwenye mishahara
(Paye), ikipungua.
“Mimi na wenzangu serikalini hatuna upungufu wa
dhamira ya kufanya hivyo, tumethibitisha miaka iliyopita na tutaendelea
kuwa hivyo,” alisema.
Huku akishangiliwa na wafanyakazi waliofurika
katika Uwanja wa Uhuru, Rais Kikwete alisema: “Najua kuwa nyongeza
tuliyotoa mwaka jana si kubwa kama wafanyakazi walivyotaka iwe... hata
mimi nisingependa iwe hivyo.”
“Kwa nyongeza iliyofanywa mwaka jana, hivi sasa
Serikali inatumia asilimia 44.9 ya Bajeti kulipa mishahara ambayo ni
asilimia 10 ya Pato la Taifa.”
Akifafanua namna Serikali ilivyofikia uamuzi wa
kuongeza mishahara kwa mwaka huu, Rais Kikwete alisema kulikuwa na
mjadala mkali baina ya wafadhili waliodai nyongeza ni kubwa mno.
“Ni kweli mapato yetu ni madogo lakini kwa kuwa
mishahara ni midogo, lazima tuendelee kuongeza, hata hicho kidogo lazima
ukitoe ili uijenge ile nafuu, alisema bila kutaja kiwango
kitakachoongozwa.
“Hata sasa kumekuwa na ubishi mkali kati ya Wizara
ya Utumishi na Hazina kuhusu nyongeza ya mwaka huu iwe mpaka kiasi
gani, nikaingilia kati nikakubaliana na utumishi, Hazina walikuwa
wanataka ipingue kidogo,” alisema.
Walimu na shemeji yao
Suala la mshahara lilijitokeza kwa namna nyingine
kwenye maandamano ya wafanyakazi pale walimu walipoamua kusimama mbele
ya jukwaa kuu na kumweleza Rais Kikwete ambaye walimtaja kama shemeji
yao, kwamba hawajapata mshahara wa Aprili wakimtaka aingilie kati.
“Shemeji, shemeji, shemeji, hatujapata mishahara yetu ya Aprili, tunaomba utusaidie,” walitoa ujumbe huo kwa njia ya wimbo.
0 Comments