DALADALA 1,800 zinazofanya safari zake kati ya Kimara na Kivukoni,
zinatarajiwa kuondolewa katika barabara hiyo yenye wateja wengi, baada
ya kuanza kwa awamu ya kwanza ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi (Dart).
Daladala hizo zitapangiwa njia nyingine za pembezoni, ambako hakuna
wateja, kama barabara ya awali, huku madereva wake watakaojitokeza
kuomba ajira, watapewa kipaumbele katika mabasi ya kasi.
Meneja Uendeshaji wa Dart, Peter Munuo, alisema hayo jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu maendeleo ya mradi huo.
“Daladala hizo zitapangiwa ruti mpya, kama mnavyojua hapa kwetu (Dar
es Salaam) usafiri ni wa tabu kidogo, hasa kwa maeneo ambayo yako
pembezoni,” alisema Munuo.
Meneja Msimamizi wa Matumizi ya Barabara wa Dart, Mohamed Kuganda, alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika mwaka kesho.
Lakini, alisema jambo hilo litawezekana, endapo mkandarasi aliyepewa
zabuni hiyo, Kampuni ya Strabag, atakomesha migogoro inayoendelea.
Alisema kwa sasa kampuni hiyo, imekuwa ikiingia katika migogoro na
wafanyakazi wake, jambo ambalo kama kampuni hiyo haitachukua hatua za
haraka, linaweza kukwamisha mradi huo kukamilika kwa wakati.
“Tunataka wakae na wafanyakazi wao, wajadili kwa sababu migogoro hii,
inaathiri maendeleo ya mradi wakati mitambo ipo, lakini haifanyi kazi
na hivyo inaweza kuchelewesha kazi,” alisema Kuganda.
Alisema mradi huo, unakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo
maandalizi ya huduma za awali. Alisema kuwa wanatarajia kuanza kutoa
huduma za awali kwa mabasi makubwa 20 na madogo 10.
Alisema zinahitajika Sh bilioni 20 ili kufanikisha hatua za awali za kuanza mradi huo.
Meneja Uhusiano wa Dart, William Gatamba, alisema madereva daladala,
watakaopewa vipaumbele watapelekwa katika mafunzo maalumu, ambapo baada
ya hapo vigezo ndiyo vitawawezesha kupata ajira.
0 Comments